Wadau wa usawa wa kijinsia wilayani Bahi mkoani Dodoma wameweka msisitizo wa kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji wa Serikali, jamii na mashirika ya kiraia katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine katika kupata haki na kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

Hayo yamesemwa Septemba 21, 2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Equality for Growth (EFG), Theresia Jeremiah Tuju, wakati wa Mdahalo wa Wadau kuhusu Kujenga Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake uliofanyika wilayani Bahi kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja, unaotekelezwa na EFG kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation Tanzania na kufadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.

Tuju amesema mdahalo huo umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kueleza changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu na kuweka mapendekezo ya pamoja yanayoweza kutekelezwa katika kukuza usawa wa kijinsia.

Amesema mjadala huo umejikita pia katika kuongeza uwajibikaji wa kila mdau katika kulinda haki za wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, huku maeneo yaliyosisitizwa yakihusisha upatikanaji na umiliki wa ardhi na mali, fursa za kiuchumi, ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi pamoja na mila na mitazamo inayokwamisha usawa.

Msaidizi wa Kisheria kutoka Bahi, Jackline Wiliam, amesema baadhi ya wananchi wameendelea kukumbana na changamoto katika kufikia haki kutokana na uelewa mdogo wa sheria na taratibu za kufuata, kushindwa kumudu gharama za huduma za kisheria, hofu na vitisho, mila na desturi kandamizi pamoja na umbali wa huduma za msaada wa kisheria.

Aidha, washiriki wa mdahalo huo wameibua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, ikiwemo unyanyapaa na kufichwa na baadhi ya wazazi kutokana na imani potofu kwamba ulemavu ni laana, huku wakisisitiza umuhimu wa watoto hao kupewa nafasi ya kupata haki, elimu, huduma na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Afisa Mradi wa Tuinuke Pamoja, Erick Kisiga, amesema mijadala mbalimbali iliyofanywa na mradi huo imebaini changamoto za wanawake kunyimwa au kuzuiwa kurithi mali katika familia walikozaliwa na walizoolewa, vikwazo katika umiliki wa ardhi na mali, mgawanyo usio sawa wa majukumu ya kaya, fursa zisizo sawa za elimu kwa wasichana, ndoa za utotoni na ushiriki mdogo wa wanawake katika maamuzi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Jane Ng’ondi, amesema Halmashauri imeendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki na wajibu katika masuala ya ardhi, mali na mirathi, pamoja na kuimarisha mazingira ya ushiriki wa wanawake na watu wenye ulemavu katika maendeleo.

Ng’ondi amesema Serikali za Mitaa na viongozi wa jamii wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na huduma kwa wakati, huku akiwataka viongozi wa dini, wazee maarufu na wadau wengine kuendelea kuelimisha jamii kuhusu utu, haki na usawa.

Amesema mdahalo huo umeweka msingi wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kugeuza changamoto na mapendekezo yaliyotolewa na jamii kuwa hatua zinazotekelezeka, ili kujenga jamii yenye usawa na kuhakikisha wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine wanapata fursa sawa za kushiriki na kunufaika na maendeleo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...