Jumla ya wananchi 3,879 wamenufaika na Kambi Maalum ya Matibabu na Upasuaji wa Macho iliyoendeshwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Qatar Charity, iliyohitimishwa leo Septemba 4, 2026 katika viwanja vya Kituo cha Afya Sebuleni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuhitimisha kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Mohammed Ali Abdalla, amesema huduma hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa matibabu ya macho Zanzibar kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao na kueleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini ushirikiano na Muhimbili na Qatar Charity katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
“Leo tunashuhudia maelfu ya wananchi wakirejeshewa matumaini ya kuona. Ushirikiano huu umeonesha kuwa tukifanya kazi pamoja tunaweza kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza adha ya kusafiri kutafuta matibabu." amesema Mhe. AbdallaKwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amesema mafanikio ya kambi hiyo yanadhihirisha dhamira ya Muhimbili ya kuwafikishia Watanzania huduma za kibingwa popote zilipo hitajika, huku akiwapongeza madaktari na watumishi wote walioshiriki kufanikisha zoezi hilo.
“Muhimbili itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya. Furaha yetu kubwa ni kuona mamia ya wagonjwa wakirejea nyumbani wakiwa wamepata tena uwezo wa kuona na kuanza maisha mapya.” ameeleza Dkt. Kimambo
Kambi hiyo ilianza Agosti 29 hadi 31, 2026 katika Kituo cha Afya Kinduni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo wananchi 971 walifanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya magonjwa mbalimbali ya macho, huku 136 wakifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho. Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, huduma zilihamishiwa Kituo cha Afya Sebuleni kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2026, ambako wagonjwa 2,769 walihudumiwa na 237 kufanyiwa upasuaji.
Kwa kipindi chote cha siku saba, jumla ya wananchi 6880 wameonwa, 3,879 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya macho, 378 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo na 406 walipatiwa miwani bila malipo. Upasuaji huo ulifanyika kwa kutumia gari maalum la upasuaji, ikiwa ni mara ya kwanza nchini Tanzania huduma hiyo kutolewa kwa mfumo huo wa kisasa.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...