SERIKALI Mkoa wa Pwani imetoa wito kwa wataalamu wa maafa kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa jamii, hususan wakulima, wafugaji na wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni, kuhusu tahadhari na hatua za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, wakati wa kikao cha Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa Mkoa wa Pwani, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa namna ya kujikinga na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Kayombo ameeleza Mkoa umeanza maandalizi ya kukabiliana na El Niño, ikiwemo kuimarisha mifumo ya mawasiliano, ufuatiliaji, maandalizi na mwitikio wa haraka, huku akizitaka halmashauri kuanza kusafisha mifereji ya maji katika maeneo mbalimbali .

Kadhalika amefafanua mkoa umetekeleza maelekezo ya Serikali ya kuanzisha Kituo cha Uendeshaji wa Dharura (EOC), kitakachosaidia kukusanya na kuchambua taarifa za majanga, hali ya hewa, maeneo hatarishi na madhara yanayotokea, pamoja na kuratibu shughuli za uokoaji, misaada na utoaji wa taarifa kwa haraka.

Aidha, Kayombo amesema Mkoa unapaswa kuwa na msimamo mmoja katika kutekeleza maelekezo ya Serikali, ikiwemo kutumia fursa ya Pwani kuwa kituo cha kuhifadhi vifaa vya dharura vya miundombinu ya barabara, huku akisisitiza ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kamati ya Maafa Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema halmashauri zote tisa na taasisi mbalimbali zimeandaa mikakati ya kukabiliana na El Niño, huku elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu kujilinda, kuchukua tahadhari, kupunguza madhara, mwitikio wa haraka na kurejesha huduma pindi athari zitakapotokea.

Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Romwald Mwendi, ameeleza Mkoa umejiandaa kwa rasilimali za dharura zikiwemo magari, boti, vifaa vya uokoaji, magari ya wagonjwa, dawa, chakula, maji, mafuta, mahema, ghala la chakula pamoja na vifaa vya mawasiliano.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...