Na. Benny Mwaipaja, Mangapwani, ZANZIBAR.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Shirika la Bandari Zanzibar, kuanza mapema maandalizi ya vifaa, mifumo na watumishi watakaohitajika kutoa huduma katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani ili kuhakikisha inaanza kufanya kazi kwa ufanisi mara tu ujenzi wake utakapokamilika.
Mhe. Balozi Omar ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake katika Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo.ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Amesema Bandari ya Mangapwani ni miundombinu muhimu ya kimkakati kutokana na uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa ujenzi wake utakapo kamilika mwaka 2028, hivyo inatarajiwa kuwa kituo muhimu cha shughuli za forodha na chanzo cha mapato ya Serikali kupitia ushuru wa forodha.
“Pamoja na ujenzi wa miundombinu ya bandari, ni muhimu taasisi zote zinazohusika na utoaji wa huduma kuhakikisha zinapanga kwa pamoja mahitaji yao ili kuepusha bandari kukamilika huku vifaa na mifumo muhimu ya uendeshaji ikiwa haijakamilika” alisema Mhe. Balozi Omar
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Shirika la Bandari Zanzibar na TRA kuoanisha ratiba zao za utekelezaji ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati na shughuli za bandari zinafanyika kwa ufanisi.
Mhe. Balozi Omar alieleza kuridhishwa na taarifa ya maendeleo ya mradi iliyobainisha kuwa ujenzi umefikia takribani asilimia 20, hatua inayolingana na matarajio ya utekelezaji kwa kipindi husika, huku mkandarasi akiendelea na kazi katika eneo la mradi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis, amesema Bandari Jumuishi ya Mangapwani ni miongoni mwa miradi muhimu inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kuimarisha shughuli za biashara na usafirishaji wa shehena ya mizigo.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni muhimu katika kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kitovu cha biashara na inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi.
Bw. Khamis alieleza kuwa ziara ya Waziri wa Fedha imekuwa fursa ya taasisi husika kujadili maendeleo ya ujenzi, kutambua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati ya mapema ya kukamilisha maandalizi ya miundombinu na huduma zitakazohitajika bandarini hapo.
Alitaja baadhi ya mahitaji muhimu kuwa ni miundombinu ya kuhifadhi mizigo, vifaa vya ukaguzi wa mizigo ikiwemo midaki (scanners), pamoja na mifumo na vifaa vya TRA, vitakavyowezesha shughuli za forodha na usafirishaji wa mizigo ya transshipment kufanyika kwa ufanisi na bila usumbufu usio wa lazima.
“Bandari hii ya Mangapwani inatarajiwa kukamilika Septemba 2028 na kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na awamu ya kwanza itakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani makontena 250,000 hadi 300,000 kwa mwaka, pamoja na tani 500,000 hadi milioni moja za mizigo ya kawaida isiyohifadhiwa kwenye makontena” alisema Bw. Khamis.
Aliongeza kuwa bandari hiyo ina uwezo wa kupanuliwa katika awamu zijazo kupitia upanuzi wa maeneo ya kuhifadhi mizigo na miundombinu mingine, hatua itakayoongeza uwezo wake wa kuhudumia biashara na mizigo kwa kadiri mahitaji yatakavyoongezeka.
Bw. Khamis alisema ujenzi wa bandari hiyo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa Zanzibar katika kuhudumia biashara ya kimataifa, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kufungua fursa mpya za uwekezaji, na Kukamilika kwa mradi huo, sambamba na maandalizi ya mapema ya taasisi zinazohusika, kunatarajiwa kuweka mazingira bora ya uendeshaji wa bandari na kuongeza mchango wake katika mapato na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis (kulia), wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto), akizungumza jambo wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo. Wa pili kushoto ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Bw. Mcha Hassan Mcha, na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis (kulia).
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Zanzibar)
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto), akizungumza jambo wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo. Wa pili kushoto ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Bw. Mcha Hassan Mcha, na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis (kulia).
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Zanzibar)








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...