Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina imani na matumaini makubwa kwa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar linaloundwa chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Aidha, CCM kimewataka Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka CCM na ACT-Wazalendo kuthamini dhamana waliyopewa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, na kuhakikisha wanalinda heshima ya nyadhifa hizo kwa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kisiwandui, Unguja.

Mbeto alisema Mawaziri na Manaibu Mawaziri wote wana wajibu wa kulinda heshima waliyopewa na Rais kwa kuitumikia Serikali na wananchi, pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Zanzibar.

Alisema baada ya uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Mawaziri, jukumu kubwa lililopo katika kila Wizara ni kumsaidia Rais kutekeleza malengo ya kisera ya Serikali kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi.

“Tunampongeza kwa dhati Rais Dk. Mwinyi kwa uteuzi na mabadiliko madogo aliyoyafanya katika Baraza lake la Mawaziri. Kuna Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka CCM na ACT-Wazalendo. Tunachowahimiza ni wakawatumikie wananchi wote,” alisema Mbeto.

Akifafanua zaidi, Mbeto alisema kila Waziri aliyepewa dhamana ana wajibu wa kupigania maslahi ya umma na kuitumikia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa utii, uzalendo na uaminifu mkubwa.

“Utaratibu mzima wa kuendesha Serikali unafahamika. Kila Waziri mwenye dhamana ana wajibu wa kutekeleza majukumu ya kisera. Macho ya Wazanzibari yanawatazama wao,” alisema.

Mbeto alisisitiza kuwa huo ni wakati wa kuithibitishia dunia kwamba tofauti na tashwishi za kisiasa zinaweza kuwekwa kando ili kuruhusu Serikali na wananchi kuendelea na shughuli za maendeleo bila mivutano.

“Twendeni tukajenge nchi. Maendeleo yanapotokea hayana alama ya CCM wala ACT-Wazalendo. Itapendeza Mawaziri wetu wakimudu kutenganisha siasa na shime ya maendeleo,” alisisitiza.

Akizungumzia kwa undani zaidi, Mbeto alisema maendeleo ya nchi hayana alama ya kisiasa wala kiitikadi, kwa kuwa maendeleo ya kisekta yanaposhika kasi hunufaisha wananchi wote bila kujali itikadi au chama cha siasa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...