Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Mwl. Protas Magesa, amewataka walimu kuwa wabunifu na kuzingatia ubora wa kazi katika utekelezaji wa mitaala na sera mbalimbali za elimu, huku akiiomba Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu na kutatua changamoto zinazowakabili walimu katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza leo Oktoba 3, 2026 jijini Dodoma kuelekea kilele cha Siku ya Walimu Duniani, Mwl. Protas amesema walimu wanahitaji kupata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kukabiliana na mabadiliko ya mtaala mpya unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwakani.
Amesema maandalizi hayo pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu yatasaidia kupunguza changamoto katika kuwahudumia wanafunzi, hasa kutokana na ongezeko la majukumu litakaloweza kujitokeza katika utekelezaji wa mtaala huo.
“Sisi kama CWT tunaamini walimu wetu wakiendelea kupata mafunzo mbalimbali kuhusiana na namna ya kukabili mtaala mpya mwakani pamoja na kuweka miundombinu mizuri, itasaidia kuondoa wakati mgumu wa kuhudumia wanafunzi".
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma CWT, Mwl. Alfred Kusaga, ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa walimu kwa kuimarisha miundombinu ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu bora.
Mwl. Kusaga amesema utekelezaji wa mipango mbalimbali katika sekta ya elimu, hususan mtaala mpya unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwakani, unahitaji maandalizi ya mapema kutokana na uwezekano wa kusababisha ongezeko la wanafunzi na hivyo kuongeza majukumu kwa walimu.
“Mabadiliko hayo yatapelekea ongezeko la kazi kwa walimu. Tunaiomba Serikali tunapozungumza kusimama pamoja kuinua na kuipa hadhi taaluma ya ualimu. Tunatamani iangalie mapema taratibu nzuri ili kila kitu kifanyike kwa ufasaha ili walimu hadhi yao iheshimike kama taaluma zingine zinavyoheshimika kwa jamii".
Naye Kaimu Mtunza Hazina Taifa wa CWT, Mwl. James Asagwile, amewahimiza walimu kuwa na ustahimilivu katika kutekeleza majukumu yao, huku akieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakihitaji ongezeko la mishahara.
Siku ya Walimu Duniani huadhimishwa kila Oktoba 5, ambapo mwaka 2026 inaadhimishwa kwa kaulimbiu inayohimiza kusimama pamoja katika kulinda taaluma, kuendeleza hadhi ya ualimu na kuangalia mustakabali wa taaluma ya ualimu kwa ujumla.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...