NA DENIS MLOWE - MVOMERO 


MKUU wa Wilaya ya Mvomero, Richard Kasesela, amewahimiza wanawake wa wilaya hiyo kutumia rasilimali walizonazo kujitengenezea mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara, badala ya kusubiri mikopo kutoka taasisi za kifedha zenye masharti, huku akiwataka kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha ili kujikwamua kiuchumi.

Kasesela ametoa rai hiyo wakati akifungua Kongamano la Wanawake wa Tarafa ya Mlali lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, akisisitiza kuwa mtaji haupaswi kutazamwa kwa upande wa fedha pekee, bali pia thamani ya vitu ambavyo mtu anamiliki lakini havitumiki ipasavyo.

Amesema wanawake wanaweza kuanza kujikusanyia mitaji kwa kuuza vitu vilivyohifadhiwa majumbani kwa muda mrefu bila kutumika, vikiwemo nguo, viatu na vitu vingine vyenye thamani, kisha kuelekeza fedha watakazopata katika shughuli za uzalishaji na biashara.

“Si kwamba vitu hivyo havina thamani, vina thamani lakini havina tija kama havitumiki. Kwa nini usivitoe ukaviuza na kupata mtaji wa kuanzia?” amesisitiza Kasesela.

Akieleza uzoefu wake binafsi, Kasesela amesema aliwahi kuuza nguo alizokuwa hazitumii na kupata karibu shilingi laki tatu na zaidi, akibainisha kuwa hatua hiyo inaonesha namna rasilimali zilizopo majumbani zinavyoweza kuwa chanzo cha mtaji wa kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Aidha, amewataka wanawake kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kupanga bajeti kabla ya kuanza shughuli za kila siku na kuepuka manunuzi yasiyokuwa kwenye mipango yao, akieleza kuwa matumizi yasiyopangwa yanaweza kuzuia fedha ambazo zingetumika kujenga mtaji.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya Mlali, Rachael Kingu, amesema changamoto zinazowakabili wanawake wengi ni pamoja na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara, pamoja na kukosa elimu kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao.

Amesema kongamano hilo limelenga kuwapatia wanawake elimu kuhusu fursa hizo ili kuwawezesha kuzitumia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Naye Diwani wa Kata ya Mzumbe, Stanslaus Matangalu, ameshukuru Serikali kwa juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi maalumu.

Matangalu amesema katika Kata ya Mzumbe, zaidi ya shilingi milioni 100 zimetolewa kwa vikundi sita vya wanawake, vikundi viwili vya vijana na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu.

Katika kongamano hilo, washiriki wamepatiwa elimu kuhusu fursa za kiuchumi na masuala mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa taasisi zilizoshiriki, zikiwemo Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), SAT, Benki ya CRDB na Benki ya NMB.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...