Na Mwandishi Wetu
Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Mpango wa Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Uziduaji (EITI Global Conference 2026) umefunguliwa rasmi mjini Brussels, Ubelgiji, ukiwakutanisha wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 57 zinazotekeleza vigezo vya EITI kwa lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia.
Akifungua mkutano huo leo Oktoba 8, 2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Kimataifa ya EITI anayemaliza muda wake, Rt. Helen Clark, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, kampuni zinazojihusisha na sekta ya uziduaji pamoja na asasi za kiraia, akieleza kuwa mshikamano wa wadau hao ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi na nchi husika kwa ujumla.
Clark, aliyeiongoza Bodi ya EITI kwa kipindi cha miaka saba, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa viwango vya EITI ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa EITI, Maria van der Hoeven, ameahidi kushirikiana na nchi wanachama katika kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya EITI. Anatarajiwa kuiongoza Bodi ya taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2029.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Uziduaji Tanzania (TEITI), Balozi Wilson Masilingi, amekutana na Katibu Mtendaji wa EITI, Mark Robinson, aliyeipongeza Tanzania kwa hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza shughuli za taasisi hiyo.
Robinson ameeleza kuridhishwa na jitihada za Tanzania katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji, huku akipongeza matumizi ya wataalamu wa ndani katika kuandaa ripoti za TEITI za kila mwaka, hatua inayochangia kuimarisha uwezo wa kitaifa katika kusimamia utekelezaji wa vigezo vya EITI.
Tanzania pia imeshiriki katika maonesho yanayoambatana na mkutano huo, yaliyotoa fursa kwa nchi wanachama kuonesha bidhaa, huduma na mbinu mbalimbali wanazotumia kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji.
Miongoni mwa masuala yanayopewa uzito katika mkutano huo ni ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia. Tanzania inatarajiwa kufanyiwa tathmini ya utekelezaji wa shughuli za EITI mwezi Julai 2027.
Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 9, 2026, ukiwa na lengo la kuimarisha uelewa na ushirikiano wa nchi wanachama katika kuhakikisha rasilimali za uziduaji zinasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji kwa manufaa ya wananchi.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...