Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetaka kuimarishwa na kuunganishwa kwa mifumo ya taarifa za taasisi mbalimbali ili kudhibiti matumizi ya taarifa za kughushi, kupunguza makosa na kuhakikisha mikopo inatolewa kwa wanafunzi wanaostahili kwa wakati.

Wito huo umetolewa leo, Oktoba 9, 2026, jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, HESLB pamoja na Wathibiti Ubora wa Elimu kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Dkt. Kiwia amesema upatikanaji wa taarifa sahihi na zinazoweza kuhakikiwa ni msingi muhimu katika kuboresha mchakato wa utoaji mikopo, ikiwemo kupanga bajeti na kuhakikisha fedha zinagawiwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wanafunzi.

Ameeleza kuwa taarifa kuhusu matokeo ya mitihani, hali ya uyatima, ulemavu na mahitaji maalumu ya wanafunzi zina nafasi muhimu katika kutambua waombaji wanaostahili kupata mikopo na msaada wa kifedha.

Aidha, amesema kuunganisha mifumo ya taarifa za taasisi husika kutarahisisha ukusanyaji na uhakiki wa taarifa, kupunguza usumbufu kwa waombaji na kusaidia wanafunzi kupata mikopo au fedha zao kwa wakati wanaporipoti katika vyuo wanavyopangiwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 787.4 kwa ajili ya mikopo na msaada kwa wanafunzi katika mwaka huu, huku zaidi ya wanafunzi 292,400 wakitarajiwa kunufaika.

Amesema wanufaika hao wanajumuisha wanafunzi wapya zaidi ya 81,300, wanafunzi 160,738 wanaoendelea na masomo pamoja na zaidi ya wanafunzi 11,000 wa ngazi ya stashahada.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ephraim Simbeye, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika katika kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinakusanywa na kuhakikiwa kwa usahihi.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha mikopo inawafikia wanafunzi wanaokidhi vigezo, huku ukisaidia kuimarisha ufanisi na uwazi katika mchakato wa utoaji mikopo ya elimu ya juu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...