Umoja wa Mabalozi Wastaafu Tanzania umeridhishwa na uwekezaji wa Serikali katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ikiwemo vifaa vya kisasa vya kufundishia na miundombinu bora, inayochangia kuzalisha wataalamu mahiri wa kuhudumia miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya usafirishaji nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya umoja wa mabalozi hao wastaafu Chuoni hapo iliyofanyika tarehe 23 Oktoba 2026, Katibu wa umoja huo Balozi Irene Kasyanju ameushukuru Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kwa mapokezi mazuri wakati wa ziara hiyo ambapo wamepata fursa ya kutembelea Chuo na kupata fursa ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na NIT, ikiwemo mafunzo yanayohusu usafiri wa anga,mabomba,reli na majini.
Amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa Tanzania kuandaa wataalamu wake wenyewe, badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi, huku akibainisha kuwa NIT ina nafasi kubwa katika kutoa ujuzi unaohitajika kuendesha na kuendeleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika sekta ya usafirishaji nchini ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR,ujenzi wa meli na uimarishwaji wa shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
Aidha,Balozi Kasyanje ametoa wito kwa mabalozi wa Tanzania ambao bado wanahudumu nje ya nchi kutembelea NIT ili kujionea uwekezaji na maendeleo yaliyofikiwa Chuoni hapo, akisema hatua hiyo itawasaidia kufahamu uwezo wa Tanzania katika kuzalisha wataalamu mahiri wazawa kwaajili ya kusimamia miradi ya kimkakati ya sekta ya usafirishaji
Aidha Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema Chuo kitafanyia kazi mapendekeza yote yaliyowasilishwa na mabalozi hao wastaafu ikiwemo kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa kisekta katika masuala ya usalama barabarani wakati wa hatua za ujenzi wa barabara kwa kuzingatia usalama wake kuanzia hatua ya usanifu, ujenzi hadi ukarabati wake ili kupunguza ajali.
Ziara imehusisha mabalozi wa Tanzania waliohudumu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Malawi,Cuba, Uholanzi,Uswisi,Marekani,Misri,Afrika ya Kusini,Ufaransa na Uturuki.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...