NJOMBE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Kilimo kupitia upya mfumo wa upangaji bei za mazao na kuweka bei zinazozingatia gharama halisi za uzalishaji, ili kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha wananufaika na jasho lao.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Makambako, mkoani Njombe, akiwa njiani kuelekea mkoani Iringa.

Amesema ni muhimu Serikali kuhakikisha bei zinazotangazwa zinamwezesha mkulima kurejesha gharama za uzalishaji na kupata faida, badala ya kuwaacha wafanyabiashara wa kati wakinufaika zaidi na mazao hayo.

Akitolea mfano wa uzalishaji wa zao la mahindi, amesema mkulima hutumia kati ya shilingi 600,000 hadi 700,000 kulima ekari moja, huku akivuna wastani wa gunia 10 hadi 20, hali inayofanya bei ya shilingi 450 hadi 500 kwa kilo kutokidhi kikamilifu gharama za uzalishaji kwa baadhi ya wakulima.

Ameeleza kuwa gharama hizo zinaweza kufikia kati ya shilingi 390 hadi 450 kwa kilo, kutegemea kiwango cha mavuno, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa bei unaomlinda mkulima mdogo dhidi ya hasara.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Kilimo kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha wakala huo unatekeleza jukumu la kuimarisha usalama wa chakula na kudhibiti kuyumba kwa bei za mazao, sambamba na kulinda kipato cha wakulima.

Amesema mfumo wa sasa wa ununuzi unapaswa kuangaliwa upya ili kuzuia wafanyabiashara wa kati kununua mazao kwa bei ya chini kutoka kwa wakulima na kuyauza kwa bei ya juu kwa NFRA, huku wakulima ambao ndiyo wazalishaji wakibaki na faida ndogo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu utakaowawezesha wakulima kuuza mazao yao moja kwa moja kwa NFRA, hatua itakayosaidia kuongeza kipato chao na kuimarisha uchumi wa kilimo.

Ameongeza kuwa maelekezo hayo yanaendana na dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli zao za uzalishaji, pamoja na juhudi za Serikali za kuimarisha uwezo wa NFRA katika ununuzi na uhifadhi wa mazao.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amekiri kuwapo kwa changamoto katika mfumo wa bei za mazao na kueleza kuwa wataalamu wa Wizara hiyo tayari wameanza kufanya tathmini ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Amesema baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, Serikali itachukua hatua zinazostahili kuhakikisha bei za mazao zinazingatia maslahi ya wakulima na uhalisia wa gharama za uzalishaji.

Kuhusu ongezeko la bei za mbolea, Chongolo amesema hali hiyo imechangiwa na changamoto za kiuchumi na migogoro inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, ambayo imeathiri gharama za uzalishaji na usafirishaji wa pembejeo za kilimo.

Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya mbolea na kuweka bei elekezi kulingana na maeneo ya usambazaji, ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wakulima.

Ameonya kuwa wafanyabiashara watakaobainika kuuza mbolea kwa bei zinazozidi viwango vilivyoelekezwa na Serikali watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria zinazotumika.

Akizungumza katika hadhara hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi, amesema ongezeko la matukio ya mauaji katika Mkoa wa Njombe limebainika kusababishwa na visa mbalimbali ikiwemo masuala ya migogoro ya ardhi na mashamba, wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.

Amewaasa wananchi wa Mkoa wa Njombe kuwa waangalifu katika masuala ya mahusiano ya mapenzi na kuepukana na tabia za kujichukulia sheria mkononi. Pia amewasihi kuachana na tabia za kuamini katika ushirikina kwani hata waganga wa kienyeji na wao wanachangamoto ambazo wanamtegemea Mungu kuzitatua.

Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amesema kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji na umeme pamoja na masoko ya mazao kutasaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za biashara na kuboresha ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Njombe.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali, zikiwemo Kilimo, Maji, Ujenzi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI na Mambo ya Ndani ya Nchi, ambao wamejibu hoja zilizowasilishwa na wabunge wa Mkoa wa Njombe na kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kutatua changamoto za wananchi.

Ziara hiyo imeweka msisitizo katika kuimarisha sekta ya kilimo, kuboresha miundombinu na kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.











Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...