Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 katika eneo la Rujewa, mkoani Mbeya, wenye thamani ya shilingi bilioni 105.7, unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya laki tano wa miji ya Rujewa, Wanging’ombe na Makambako.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama, sambamba na kutekeleza azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameipongeza Wizara ya Maji kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo, huku akiwataka wataalamu na watendaji wanaohusika kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na kutatua changamoto zinazojitokeza bila kuchelewa, akielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha maeneo yanayokabiliwa na upungufu wa huduma hiyo yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu, sambamba na kuchukua hatua za dharura pale inapohitajika ili kupunguza adha wanayoipata wananchi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha miradi inayotekelezwa inatoa matokeo yanayoonekana kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu, matumizi sahihi ya fedha na uwajibikaji wa watendaji katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati, huku akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuona matokeo badala ya michakato inayochelewesha upatikanaji wa huduma.
Amesema Wizara ya Maji itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
Aidha, Waziri Aweso ameahidi kuhakikisha shilingi bilioni moja zinapatikana kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Maji wa Chimala, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65 lakini umekabiliwa na changamoto ya fedha.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais ya kuhakikisha miradi ya maji inayokabiliwa na changamoto inakamilishwa ili wananchi wapate huduma kwa wakati.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rujewa, Mhandisi Lestus M. Linda amesema mradi huo umefikia wastani wa asilimia 80 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Novemba 2026.
Amesema mradi huo unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama katika miji ya Rujewa, Wanging’ombe na Makambako, ambako mahitaji ya maji yameendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu na shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Linda, kwa sasa miji hiyo mitatu inazalisha jumla ya lita 8,706,000 za maji kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji ya lita 30,141,000, hali inayosababisha upungufu mkubwa wa maji.
Amefafanua kuwa mradi huo utatumia Mto Mbarali kama chanzo cha maji na utakuwa na uwezo wa kuzalisha na kutibu lita milioni 40 kwa siku, ambapo lita milioni 15 zitatumika kuhudumia Rujewa na lita milioni 25 zitaelekezwa Wanging’ombe na Makambako.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa Aprili 2023 unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, mtambo wa kutibu maji, matanki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni nane, vituo vya kusukuma maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza maji yenye urefu wa kilometa 54.4. Ujenzi wa chanzo cha maji na tanki la kuhifadhi lita milioni tano umefikia asilimia 95, mtambo wa kutibu maji asilimia 88, huku ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji kutoka Rujewa kupitia Wanging’ombe hadi Makambako ukifikia asilimia 90. Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Larsen and Toubro Construction Limited ya India chini ya usimamizi wa kampuni ya Wapcos Limited.
Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa majisafi na salama, hatua ambayo inaunga mkono dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 ya wananchi katika maeneo ya mijini.
Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya, ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, uwajibikaji wa watendaji na kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na huduma zinazotolewa na Serikali.




.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...