Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph, amesema wizi wa mita za maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili mamlaka hiyo, baada ya zaidi ya mita 100 kuibwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Amesema takwimu za DUWASA zinaonesha kuwa vitendo hivyo vinaendelea kuwa changamoto katika usimamizi wa huduma za maji, huku baadhi ya vifaa vinavyoibwa vikidaiwa kutumika kwa shughuli nyingine zisizohusiana na matumizi yake ya awali.

Mhandisi Joseph, ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma katika Mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema ufuatiliaji uliofanywa umebaini kuwa baadhi ya mita hizo hutumika kutengeneza bangili, huku nyingine zikiishia kuuzwa kama vyuma chakavu. Hali hiyo inaibua wasiwasi kuhusu uharibifu wa vifaa vinavyotumika katika utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, DUWASA imekubaliana na baadhi ya wateja kufunga mita za maji ndani ya nyumba au katika maeneo yenye ulinzi, ikiwa ni hatua ya kupunguza uwezekano wa vifaa hivyo kuibwa. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mita zinakuwa salama huku mamlaka ikiendelea kutoa huduma kwa wateja wake.

Hata hivyo, Mhandisi Joseph amesema utaratibu wa kufunga mita ndani ya nyumba nao una changamoto zake, hasa pale watumishi wa DUWASA wanapohitaji kuingia katika maeneo ya wateja kwa ajili ya kufanya usomaji wa mita. Amesema baadhi ya wananchi hawatoi ushirikiano unaohitajika, hali inayowapa watumishi hao wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao.

Ameeleza kuwa katika baadhi ya matukio, watumishi wanaofika kufanya usomaji wa mita hukumbana na mazingira yasiyo rafiki, ikiwemo kufunguliwa mbwa, jambo linaloweza kuwazuia kutekeleza majukumu yao kwa urahisi. Kutokana na hali hiyo, ushirikiano wa wananchi unahitajika katika kulinda mita za maji, kurahisisha usomaji wake na kuimarisha utoaji wa huduma. DUWASA inaendelea kukabiliwa na jukumu la kuhakikisha vifaa hivyo vinalindwa dhidi ya wizi huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa watumishi wake.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...