Na Janeth Raphael – MichuziTV

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Ndugu Agrey Mwanri, amewataka watumishi wa Serikali wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kuhakikisha uwekezaji katika majengo na miundombinu ya kisasa unaendana na utoaji wa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Mwanri ametoa wito huo leo, Oktoba 29, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya majengo ya wizara na taasisi za Serikali zilizopo Mtumba, akisisitiza kuwa majengo ya kisasa pekee hayatoshi bila uwajibikaji na utendaji bora wa watumishi.

Amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu hiyo unapaswa kuonekana kupitia huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo kuwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Aidha, amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupewa kipaumbele kwa kusikilizwa, kuhudumiwa kwa heshima na kupata huduma kwa wakati, kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa mazingira bora ya kufanyia kazi yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza tija na ufanisi katika utendaji wa Serikali, badala ya kuishia katika mwonekano mzuri wa majengo na miundombinu pekee.

Ziara hiyo ni sehemu ya kutembelea majengo ya wizara na taasisi za Serikali zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, huku msisitizo ukiwa ni kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu unaambatana na huduma bora zinazogusa maisha ya wananchi.

Mji wa Serikali Mtumba ni eneo lililotengwa kwa ajili ya makao ya wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kurahisisha uratibu wa shughuli za Serikali.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...