Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini kwa kudhamini mashindano ya siku tatu ya Kilombero Golf Open 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya gofu vya Kilombero Sugar, mkoani Morogoro yakilenga kukuza vipaji, ushindani na ushiriki mpana katika mchezo huo.

Mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki hii yamehusisha ushiriki timu kutoka vilabu saba, ambavyo ni TPDF Lugalo, Dar es Salaam Gymkhana, Kilimanjaro Golf Club, TPC Club, Morogoro Gymkhana, Mufindi Golf Club na Kilombero Golf Club.

Akizungumzia mashindano hayo, Mkuu wa Miamala na Amana za Wateja Wakubwa wa NBC, Jimmy Myalize, alisema udhamini huo ni sehemu ya mkakati wa benki kupanua ushiriki wake katika michezo na burudani, sambamba na mchango wake wa muda mrefu kupitia Ligi Kuu ya NBC.

“Tumekuwa wadau wakubwa wa mchezo wa soka kupitia Ligi Kuu ya NBC, na mchezo wa riadha kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon. Hata hivyo bado tunaendelea kupanua wigo wa ushiriki wetu katika sekta ya michezo na burudani kwa kushiriki kwenye michezo mingine pia. Tunataka kuwa sehemu ya ukuaji wa mchezo wa gofu nchini Tanzania,” alisema Myalize.

Aliongeza kuwa NBC itaendelea kushirikiana na wadau katika shughuli zinazochochea maendeleo ya jamii, huku ikiendelea kutoa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja binafsi, makampuni na biashara ndogo na za kati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kilombero Country Club na Mkurugenzi wa Kilimo kwa Wakulima wa Kilombero Sugar, Pierre Redinger, alisema kurejea kwa mashindano hayo baada ya kusimama kwa miaka miwili ni fursa ya kuwakutanisha wachezaji na wadau, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa jamii.

“Kilombero Open si mashindano ya gofu pekee, bali pia ni fursa ya kuwakutanisha wadau wa michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii yetu. Tunataka kuhakikisha kuwa mchezo huu unakuwa jumuishi na unatoa fursa kwa watu wengi zaidi,” alisema Redinger huku akiishukuru benki ya NBC na wadau wengine kwa udhamini wao kwenye mashindano hayo.

Alisema baadhi ya wachezaji wanaoshiriki walianza kama caddies (wasaidizi wa wachezaji wa gofu) takribani miaka mitatu iliyopita na wamepiga hatua katika mchezo huo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza vipaji na kutoa nafasi kwa wanawake na makundi mengine kushiriki.

Naye Meneja wa Mahusiano na Mawasiliano wa Kilombero Sugar, Victor Byemela, alishukuru wadau wanaounga mkono mashindano hayo ikiwemo benki ya NBC na kuhimiza ushiriki zaidi wa taasisi na makampuni katika kukuza michezo nchini.

“Tunaamini michezo inatuunganisha, inatuwezesha kujenga mahusiano na kutafakari kwa pamoja namna ya kuendeleza vipaji. Tunawakaribisha wadau na wapenzi wa gofu kuendelea kuunga mkono Kilombero Golf Open 2026,” alisema Byemela.

Mwenyekiti wa Kilombero Country Club na Mkurugenzi wa Kilimo kwa Wakulima wa Kilombero Sugar, Pierre Redinger (katikati) sambamba na wadau wengine we mchezo wa golf wakiwemo wachezaji na maofisa wa benki ya NBC wakionyesha ishara ya mchezo wa golf wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mashindano ya siku tatu ya Kilombero Golf Open 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya gofu vya Kilombero Sugar, mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Benki ya NBC ni moja ya wadhamini muhimu wa mashindano hayo.

Mkuu wa Miamala na Amana za Wateja Wakubwa wa NBC, Jimmy Myalize (kusoto) akijadili jambo na Mwenyekiti wa Kilombero Country Club na Mkurugenzi wa Kilimo kwa Wakulima wa Kilombero Sugar, Pierre Redinger (kulia) wakati wa mashindano hayo.







Mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki hii yamehusisha ushiriki timu kutoka vilabu saba, ambavyo ni TPDF Lugalo, Dar es Salaam Gymkhana, Kilimanjaro Golf Club, TPC Club, Morogoro Gymkhana, Mufindi Golf Club na Kilombero Golf Club.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...