Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kushirikiana na makatibu wakuu wa Wizara zote, kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya bustani na upandaji miti katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, yanatunzwa na kuendelezwa kwa kuzingatia mpango uliowekwa.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Oktoba 30, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba.

Amesema uwepo wa maeneo ya kijani ni sehemu muhimu ya mandhari ya mji huo, hivyo ni wajibu wa viongozi na watumishi wa Serikali kuhakikisha yanakuwa na uoto wa asili unaoonekana badala ya kubaki katika mipango pekee.

Akisisitiza agizo hilo, Rais Samia amesema maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya bustani na misitu yanapaswa kuendelezwa kwa kupanda miti na kuyatunza ili kudumisha mazingira bora katika makao hayo ya Serikali.

“Agizo langu kwako Katibu Mkuu Kiongozi, ukishirikiana na makatibu wakuu wote, yale maeneo ya kijani yawe kijani kweli kweli,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika, kusimamia matumizi sahihi ya ardhi kwa kuzingatia mipango miji na kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa matumizi maalumu hayavamiwi.

Amesisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya wazi, hifadhi za barabara na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya huduma za jamii ili kuzuia matumizi holela ya ardhi yanayoweza kuathiri utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha Mtumba unakuwa mji wenye mpangilio mzuri, mandhari ya kuvutia na mazingira endelevu, huku maendeleo ya miundombinu yakienda sambamba na uhifadhi wa maeneo ya kijani na uzingatiaji wa mpango mkuu wa Jiji la Dodoma
























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...