Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

WANANCHI zaidi ya 200 wamejitokeza kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), zikiwemo za usajili na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa, katika mabanda ya maonyesho ya Kampeni ya Samia Legal Aid, Maili Moja, Kibaha.

Huduma hizo zinatolewa katika siku ya pili ya utekelezaji wa kampeni hiyo ya awamu ya pili, iliyoanza Oktoba 28 na inatarajiwa kuhitimishwa Novemba 7, 2026, ikiwa na jumla ya siku 10 za utoaji huduma mbalimbali za kisheria kwa wananchi.

Msajili Mwandamizi wa RITA Wilaya ya Kibaha, George Chuwa, alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili matukio muhimu ya kijamii na kisheria, ikiwemo vizazi, vifo, ndoa na talaka na huduma za udhamini na ufilisi.

Alieleza wananchi wanapaswa kuhakikisha watoto wanasajiliwa mara wanapozaliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa, huku akisisitiza umuhimu wa kusajili vifo kwa kuwa nyaraka hizo ni muhimu katika kulinda haki za kisheria.

Chuwa alieleza kuwa kupitia huduma hizo za karibu, majina ya waombaji huingizwa kwenye mfumo na kuchakatwa kwa haraka, huku vyeti vilivyokamilika vikikabidhiwa kwa wahusika ili kuhakikisha vinawafikia walengwa kwa wakati.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kufuata taratibu halali za kupata vyeti na kuepuka kughushi nyaraka au kutumia njia zisizo halali, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kosa la jinai.

Pia aliwahimiza wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia mapema na kusajili bodi za udhamini ili kupunguza migogoro ya kifamilia na mali.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo, akiwemo Linda Samwel, mkazi wa Tangini, na Jonathan Isack, wameishukuru kampeni hiyo kwa kusogeza huduma karibu na kurahisisha upatikanaji wa huduma ambazo awali zilihitaji kusafiri umbali mrefu na kutumia muda zaidi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...