Na Byera Deus, Biharamulo

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Nyakanazi–Nyakafundikwa, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera, analipwa Sh milioni 600 ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo unaotarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 42,000.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.9, ambao hadi sasa umefikia asilimia 78 ya utekelezaji.

Amesema kazi kubwa za ujenzi zimekamilika, huku shughuli zilizobaki zikihusisha kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma hiyo ifikapo Desemba mwaka huu, endapo malipo kwa mkandarasi yatafanyika kwa wakati.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji inayoukabili mji wa Nyakanazi, ambao unaendelea kukua kwa kasi na kuwa na mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa Nyakanazi ni eneo muhimu kiuchumi na kijiografia, likiwa lango la wageni wanaoingia na kutoka katika nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hivyo upatikanaji wa maji ya uhakika ni muhimu kwa wakazi na wageni wanaopita katika eneo hilo.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa malipo ya wakandarasi kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa, akilitaka RUWASA kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanaotekeleza miradi hiyo hawakwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Biharamulo, Mhandisi Lucas Matina, amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji na miundombinu mingine ya mradi, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili huduma iweze kutolewa kwa wananchi wa Nyakanazi na maeneo jirani.

Amesema licha ya mradi kufikia asilimia 78 ya utekelezaji, mkandarasi amelipwa Sh milioni 700 pekee kati ya gharama zote za mradi, huku akiwa anadai zaidi ya Sh bilioni 1.4, hali inayohitaji hatua za haraka ili kukamilisha kazi zilizobaki.

Naye Mkurugenzi wa Mipango wa RUWASA Makao Makuu, Mhandisi Enock Wagala, amesema wakala huo unafanyia kazi agizo la Naibu Waziri, huku Sh milioni 600 zikitarajiwa kulipwa ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi.

Amesema RUWASA inatambua umuhimu wa mradi wa Nyakanazi–Nyakafundikwa katika kutatua changamoto ya maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi, kutokana na ukuaji wa mji huo na ongezeko la mahitaji ya huduma za kijamii na kiuchumi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...