Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la Revival Education Trust limepanga kuwasaidia wanafunzi 100 kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi kurejea shuleni mwaka ujao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Akizungumza katika mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, Muasisi wa shule hiyo ambayo ndio inalisimamia shirika hilo, Diodorus Tabaro amesema mpango huo unalenga wanafunzi waliolazimika kuacha shule kutokana na changamoto za kifedha, licha ya kuwa na uwezo na vipawa vya kufanikiwa kielimu.
Amesema kati ya wanafunzi 100 watakaonufaika na mpango huo, 50 watapata nafasi za bweni, huku wengine 50 wakisoma bila kulala shuleni, ili kuwawezesha kuendelea na masomo kulingana na mazingira yao.
Tabaro ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo ya kufungua milango ya elimu kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji, akisisitiza kuwa changamoto za kiuchumi hazipaswi kuwa kikwazo cha kutotimiza ndoto za watoto.
Aidha, amesema kwa kutambua umuhimu wa kusaidia watoto wenye uhitaji, yeye binafsi ana mpango wa kugharamia masomo ya watoto saba katika mwaka wa masomo alioutaja awali, huku akiwahimiza watu wengine wenye uwezo kujitokeza kusaidia wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto hizo.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanaotoka katika familia zenye hali ngumu wanapata fursa ya elimu na kujenga maisha bora ya baadaye.
Awali mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Can Tanzania, Sixbert Mwanga ameahidi kuchangia jumla ya Sh milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kupitia Taasisi ya Revival Education Trust iliyochini ya Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, kwa lengo la kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye changamoto za kiuchumi kupata fursa ya elimu.
Mwanga amesema katika safari yake ya elimu, alikumbana na changamoto ambazo zilimfanya atambue umuhimu wa kupata msaada, akibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hukosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu za kifamilia, hata pale wanapokuwa na uwezo wa kufanya vizuri kitaaluma.
Amesema wapo wanafunzi ambao hushindwa kuendelea na masomo baada ya kutofaulu mitihani au kukosa uwezo wa kugharamia elimu, huku wengine wakipata nafasi ya kuendelea kutokana na msaada wa wazazi, ndugu au watu wengine wenye uwezo wa kifedha.
Nao baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa jambo la kusaidia baadhi ya wenzao wasiojiweza ni nzuri na wanaliunga mkono kwani lina lengo la kwenda kuwainua wale waliokata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto ya kifedha.
Wamesema wanamtakia kila la kheri aliyebuni na kuja taasisi hiyo ya kuwasaidia wanafunzi wenzao wenye changamoto hiyo ya kifedha katika familia zao.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...