Wananchi wa Kata ya Majengo, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wanatarajia kunufaika na kukamilika kwa ujenzi wa bwawa la maji la Mwambazi lililogharimu Sh2.1 bilioni, linalolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Wakizungumza kuhusu mradi huo, baadhi ya wananchi wa Kata ya Majengo wamesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mgawo wa maji, hali inayowaathiri katika shughuli zao za kila siku na kujipatia kipato.
Wamesema kukamilika kwa bwawa hilo kunatoa matumaini ya kupungua kwa changamoto hiyo na kuboresha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa kata hiyo.
Akizungumzia mradi huo, Msimamizi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa, Mhandisi Emanuel Nduiya, amesema bwawa hilo limekamilika na lina ujazo wa lita milioni 741.
Amesema bwawa hilo linatarajiwa kusambaza maji katika kata zaidi ya saba za Manispaa ya Sumbawanga, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jimboni humo, amesema mradi huo unatarajiwa kusaidia kutatua changamoto ya kukatika kwa maji mara kwa mara kwa wakazi wa maeneo husika.
Aidha, amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili kuhakikisha inaendelea kutoa huduma kwa ufanisi na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...