
Na Mwandishi Wetu - Arusha.
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA) imeandaa mafunzo ya kikanda jijini Arusha kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu kutoka nchi 16 barani Afrika katika ukusanyaji wa takwimu za kisayansi zitakazosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya wadudu aina ya mbung’o wanaosababisha kuenea kwa ugonjwa wa ndorobo kwa mifugo.
Mafunzo hayo ya wiki mbili, yanayofanyika katika Hoteli ya Best Western Parot Hotel jijini Arusha kuanzia leo Oktoba 19 hadi 30, 2026, yanalenga kuongeza ujuzi wa wataalamu katika kutambua maeneo yenye mbung’o, kukusanya na kuchambua takwimu pamoja na kupanga mikakati madhubuti ya kudhibiti wadudu hao kwa kutumia mbinu za kisasa, ikiwemo teknolojia ya nyuklia.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema mbung’o na ugonjwa wa ndorobo vinaendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya sekta ya mifugo na kilimo katika nchi nyingi za Afrika, kutokana na kusababisha vifo vya mifugo, kupungua kwa uzalishaji na kuongeza gharama za matibabu kwa wafugaji.
Prof. Najat amesema pamoja na juhudi mbalimbali zilizofanyika kwa miaka mingi, bado kuna maeneo yenye ardhi yenye rutuba ambayo hayatumiki ipasavyo kwa shughuli za kilimo na ufugaji kutokana na uwepo wa mbung’o, hali inayochangia kudhoofisha uchumi wa wananchi na kuhatarisha usalama wa chakula.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia kupitia mbinu ya kuzalisha na kuachia mbung’o dume waliohasiwa, inayojulikana kama Sterile Insect Technique (SIT), ni miongoni mwa njia muhimu zinazoweza kusaidia kupunguza idadi ya wadudu hao na hatimaye kuwaondoa katika maeneo yaliyoathirika.
“Teknolojia hii inahusisha kuzalisha mbung’o dume, kuwahasi kwa kutumia mionzi na kuwaachia katika mazingira ili wapandane na mbung’o jike wa kawaida bila kuzalisha kizazi kipya. Kwa kufanya hivyo, idadi ya mbung’o hupungua hatua kwa hatua na kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa ndorobo,” amesema Prof. Najat.
Ameongeza kuwa mafanikio ya matumizi ya teknolojia hiyo yanategemea upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu maeneo wanakopatikana mbung’o, idadi yao na mazingira wanamoishi, jambo linalofanya mafunzo hayo kuwa muhimu katika kuimarisha mipango ya kitaifa na kikanda ya kudhibiti wadudu hao.
Prof. Najat ameitaja Zanzibar kuwa mfano wa mafanikio ya matumizi ya mbinu za kisayansi katika kutokomeza mbung’o, akieleza kuwa uzoefu huo unaonesha namna ushirikiano wa taasisi, matumizi ya teknolojia na mipango endelevu vinavyoweza kuleta matokeo chanya katika sekta ya mifugo.
Amesema mafunzo hayo yanafanyika kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika katika Utafiti, Maendeleo na Mafunzo ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia (AFRA), unaosaidiwa na IAEA, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika kutumia teknolojia ya nyuklia katika kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Bwana Peter Ngamilo, amesema mafunzo hayo yanaonesha umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kushughulikia changamoto zinazogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, hususan katika sekta za kilimo na mifugo.
“Wananchi wengi wanaposikia teknolojia ya nyuklia wanaweza kufikiria matumizi yake yanahusu uzalishaji wa umeme au masuala ya silaha pekee. Ukweli ni kwamba teknolojia hii ina matumizi mengi yenye manufaa makubwa katika maisha yetu ya kila siku, ikiwemo kudhibiti wadudu waharibifu, kuboresha uzalishaji wa kilimo na mifugo na kuimarisha usalama wa chakula,” amesema Ngamilo.
Ameongeza kuwa TAEC itaendelea kushirikiana na taasisi za ndani na kimataifa katika kuhamasisha matumizi salama ya sayansi na teknolojia ya nyuklia ili kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa zinazotokana na teknolojia hiyo katika kukuza uchumi na kuboresha maisha yao.
Mafunzo hayo yanajumuisha vipindi vya nadharia na vitendo vinavyohusu maandalizi ya ukusanyaji wa takwimu za mbung’o, uandaaji wa mikakati ya uchukuaji wa sampuli na utekelezaji wa tafiti za awali katika maeneo yenye wadudu hao.
Katika mafunzo hayo, wataalamu kutoka IAEA wanashirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu wa kukabiliana na changamoto ya mbung’o barani Afrika.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia nchi zinazoshiriki kuboresha ukusanyaji wa taarifa za kisayansi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza ufanisi wa programu za kudhibiti mbung’o na ugonjwa wa ndorobo, hatua itakayochangia kulinda afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...