Na Jane Mwakyoma, Rukwa

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Abdi Mahamoud Abdi, amewataka viongozi wa chama hicho mkoani Rukwa kulinda na kuendeleza umoja na mshikamano uliopo ndani na nje ya chama ili kuhakikisha unadumu na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Abdi alimeyasema hayo Novemba 5, 2026, alipomwakilisha Mlezi wa CCM Mkoa wa Rukwa, Jamal Kassim Ali, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilicholenga kusimamia vikao vya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kupitia utekelezaji wa majukumu ya chama na Serikali pamoja na kujadili mapendekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, hivyo viongozi wa chama na Serikali wanapaswa kuudumisha kupitia utendaji wao wa kila siku.

Aidha, aliwashukuru viongozi hao kwa kuendelea kudumisha mshikamano na kuwataka kuulinda Muungano ulioasisiwa na viongozi waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume.

"Kama wasingekuwa viongozi wetu hawa wawili, Mwalimu Nyerere na Rais Karume, nchi hizi mbili zisingekuwa na Muungano huu wala umoja huu. Muungano wa ASP na TANU ndiyo uliofanya CCM kuwa hapa. Nataka kuwaambia kuwa mshikamano ndiyo msingi wetu, hasa kwa nchi yetu," alisema  Abdi 

Alisisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kujiandaa na uchaguzi ndani ya chama kwa kuhakikisha unafanyika kwa amani, utulivu na demokrasia, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga umoja uliojengwa ndani ya CCM.

"Nataka kuona mshikamano huu mlionionyesha hapa hata baada ya uchaguzi nione ukiendelezwa," alisisitiza.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Silafu Maufi, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema kikao hicho kililenga kujadili tathmini ya kazi za chama na Serikali pamoja na mapendekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Aliwataka wajumbe wa kikao hicho kujadili na kutathmini ajenda zilizowasilishwa kwa kuzingatia maslahi ya maendeleo ya taifa.

Maufi aliongeza kuwa siasa zinapotumika vizuri huwa chachu ya kujenga uchumi na kuleta maendeleo, hivyo viongozi wanapaswa kuzitumia kwa manufaa ya nchi.

"Siasa ni uchumi na siasa ni maendeleo, na ndani ya maendeleo kuna siasa," alisema Maufi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...