Zaidi ya wakazi 8,160 wa Kata ya Kwedizinga, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, wanufaika na huduma bora za mawasiliano kufuatia uzinduzi wa mnara mpya wa mawasiliano wa Airtel Tanzania, unaolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za simu na intaneti katika eneo hilo.

Miundombinu hiyo mipya itaongeza upatikanaji wa mtandao Kwedizinga na maeneo jirani, yakiwemo Ugweno na Taula, na kuwawezesha wakazi kupata huduma za kidijitali zinazosaidia shughuli za kiuchumi, elimu, upatikanaji wa taarifa na mawasiliano ya kila siku.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lydia Komnunga, Meneja Biashara wa Airtel Tanzania Kanda ya Kaskazini, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya kampuni ya kuendelea kusogeza huduma za mawasiliano karibu na wananchi Kila Kona nchini, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jamii.

"Airtel imejikita kuhakikisha tunafika kila eneo ili wananchi wapate huduma za mawasiliano zilizo bora na za uhakika Kila Kona. Uwepo wetu Kwedizinga utawawezesha wananchi kuboresha biashara zao, kupata fursa mpya za kiuchumi na kuchochea maendeleo katika vijiji na vitongoji. Uwekezaji huu pia utasaidia kufungua fursa kwa vijana na kukuza biashara katika eneo hili," alisema Lydia.


Ameongeza kuwa huduma bora za mawasiliano zitakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza shughuli za kilimo, ambazo ni miongoni mwa shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hilo, hususan kilimo cha machungwa, mkonge na mihogo.

Justina Kashisha, Mtendaji wa Kata ya Kwedizinga, alisema uwepo wa mnara huo utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi kwa kuondoa changamoto za mawasiliano zilizokuwa zikikwamisha shughuli za biashara na maendeleo ya jamii.

"Uwepo wa mnara huu wa Airtel unaashiria kufunguka kwa fursa nyingi za kiuchumi katika Kata yetu ya Kwedizinga, ambako wakazi wengi wanajishughulisha na kilimo cha machungwa, mahindi na mkonge. Kwa sasa biashara nyingi zinafanyika kupitia mifumo ya mtandao, hivyo kukosekana kwa mawasiliano kulikuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wetu. Ninaamini Kwedizinga inaingia katika hatua mpya ya maendeleo, yenye fursa nyingi za kukuza biashara na kuongeza kipato cha kaya. Tunawashukuru sana Airtel kwa kuwekeza katika kata yetu," alisema.

Kwa upande wake, Prisca Stephano, mkazi wa Kwedizinga, alisema changamoto za mawasiliano zilizokuwepo hapo awali zilikuwa zikikwamisha shughuli za wafanyabiashara, hasa katika kuwasiliana na wasambazaji na kuagiza bidhaa za biashara.

"Tunashukuru kwa uwepo wa mnara huu kwa sababu hapo awali tulikuwa tunakabiliwa na changamoto nyingi, hasa wafanyabiashara walipohitaji kuwasiliana na wasambazaji ili kuagiza bidhaa zao. Tangu mnara huu ulipojengwa, mawasiliano yamekuwa rahisi zaidi. Hata familia zinanufaika kwa sababu sasa watu wanaweza kuwasiliana na wapendwa wao bila kukatizwa na changamoto za mtandao kama ilivyokuwa awali. Tunaishukuru Airtel kwa kusikiliza mahitaji yetu na kutuletea huduma hii," alisema.

Mbali na kuchochea shughuli za kiuchumi, huduma bora za mawasiliano zinatarajiwa kuwawezesha wakazi kupata taarifa na nyenzo za kujifunzia kupitia mifumo ya kidijitali, taarifa za umma pamoja na kurahisisha mawasiliano na watoa huduma za afya, hivyo kupunguza changamoto zinazotokana na umbali wa kijiografia.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya usajili wa huduma za intaneti ilifikia milioni 62.79 kufikia Juni 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.48 ndani ya robo mwaka husika. Kiasi cha matumizi ya data pia kiliongezeka kwa asilimia 11.65 na kufikia petabyte 1,041, hali inayoonesha kuongezeka kwa umuhimu wa huduma za mawasiliano katika shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

Uzinduzi wa mnara wa Kwedizinga ni sehemu ya uwekezaji endelevu wa Airtel Tanzania katika miundombinu ya mawasiliano unaolenga kupanua wigo wa mtandao, kufikia jamii ambazo bado hazijahudumiwa kikamilifu na kuchochea maendeleo jumuishi ya kidijitali.

Kupitia upanuzi wa mtandao wake, Airtel Tanzania inaendelea kujidhatiti kusogeza huduma bora za mawasiliano na kidijitali karibu zaidi na Watanzania, kwa kuchochea maendeleo na kufungua fursa Kila Kona.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...