Na.Mwandishi Wetu – DODOMA

ALMES International School ya Dodoma imesisitiza umuhimu wa elimu bora, malezi yenye maadili na ushirikiano wa karibu kati ya shule na wazazi katika kumwandaa mtoto kuwa kiongozi bora wa baadaye, mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa mahafali ya nne ya shule hiyo yaliyofanyika, jijini Dodoma, yakihusisha wanafunzi wa Pre-Unit na Grade Seven, ambao wamehitimu hatua mbalimbali za elimu na kuelekea katika hatua nyingine za masomo.

Mmiliki wa Almes International School, Weja Ng’olo, amesema shule hiyo imeendelea kuwekeza katika elimu na malezi bora, kwa kuzingatia maadili, kumfundisha mtoto kumkumbuka Mungu, usafi na kuwa na mazingira bora ya kujifunzia, akibainisha kuwa elimu inapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya maisha.

Amesema shule hiyo inaendelea kujipanga kwa kuhakikisha inaboresha huduma zake mara kwa mara, huku ikiongeza programu za ziada zinazolenga kukuza vipaji, ujuzi na uwezo wa wanafunzi katika maeneo mbalimbali.

“Tunawashukuru sana wazazi kwa kutuamini na kutuletea watoto wao. Wazazi ni mabalozi wetu wakubwa, kwa sababu mzazi anapomweleza mzazi mwingine kuhusu huduma anazoziona kwa mtoto wake, hiyo ndiyo njia nzuri ya kuitangaza shule,” amesema Ng’olo.

Aidha amesema shule hiyo inaendelea kuboresha miundombinu, kuongeza huduma za elimu na kuimarisha programu za malezi ili kuwapatia wanafunzi elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Ng’olo amesema shule binafsi zina nafasi kubwa katika kusaidia Serikali kutoa elimu bora kwa wananchi, huku akieleza kuwa uwekezaji wa ndani katika sekta hiyo unaweza kuongeza fursa za elimu na kuwawezesha watoto wa Tanzania kushindana katika soko la elimu na ajira ndani ya Afrika Mashariki na maeneo mengine.

Hata hivyo amesema kuwa Almes ina mpango wa kuimarisha elimu ya vitendo na shughuli za ziada, ikiwamo michezo, ushonaji, muziki, kukare na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), huku ikiendelea kuboresha maabara ya kompyuta na kuangalia namna ya kujumuisha teknolojia ya akili bandia (AI) katika mafunzo.

Katika hatua nyingine, amesema shule hiyo imeanzisha programu maalumu ya kuwahudumia watoto wakati wa likizo, inayolenga kuwasaidia wazazi wanaokuwa na majukumu ya kikazi huku watoto wao wakiendelea kujifunza na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ya kimwili, kiakili na kijamii.

Amesema programu hiyo itaanza Novemba 16 hadi Desemba 16, ambapo watoto watashiriki mazoezi ya jumla, michezo ya soka, kikapu, voliboli na tenisi, pamoja na shughuli za kompyuta, muziki, kukare na nyinginezo. Ada ya programu hiyo ni Sh200,000 kwa mwezi kwa wanafunzi wa Almes na Sh250,000 kwa watoto kutoka shule nyingine.

Ng’olo amesema programu hiyo inawalenga watoto wote bila kujali shule wanazosoma, akibainisha kuwa ni fursa ya kuwapatia malezi bora, ulinzi na mazingira ya kujifunza wakati wa likizo, badala ya kukaa nyumbani bila shughuli za kuwaendeleza.

Hata hivyo, amesema shule binafsi zinazoanza kukua hukutana na changamoto mbalimbali za uendeshaji, ikiwamo kodi na michango ya taasisi mbalimbali, ambazo wakati mwingine huongeza gharama na kuwa mzigo kwa shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi.

Ameishauri Serikali kuangalia mazingira ya shule changa ili kuziwezesha kukua na kuendelea kutoa huduma bora za elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Christine Mwima, amewataka wazazi kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya elimu ya watoto kwa kufuatilia masomo, kazi za nyumbani (homework) na maendeleo yao kwa ujumla, badala ya kuliachia jukumu hilo walimu pekee. Amesema ushirikiano wa wazazi na walimu ni muhimu katika kujenga msingi imara wa elimu na maadili.

Mwima pia amesisitiza umuhimu wa wazazi kufuatilia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto wao, kuhakikisha wanaitumia kwa manufaa ya kujifunza na kujenga ujuzi, huku akibainisha kuwa malezi bora ni jukumu la pamoja kati ya familia na shule kwa kuwa watoto wa sasa ndio viongozi wa baadaye.

Naye Margreth Fabian, mzazi wa Amaris Charles, mwanafunzi wa shule hiyo, amesema ushirikiano kati ya wazazi na Almes International School umechangia kuleta mabadiliko chanya kwa watoto, hususan katika maendeleo ya masomo, uwezo wa kujieleza na mwenendo wa kitabia.

Amesema wazazi wanapaswa kuendelea kufuatilia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto na kuwaelekeza kuitumia katika shughuli zenye tija, ikiwamo kujifunza na kufanya kazi za shule.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...