Programu tumishi mpya ya simu (App) iitwayo Kunani Tizii imetambulishwa jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuwaunganisha wananchi na taarifa za ujio na uwepo wa matukio mbalimbali yanayopangwa au kufanyika kufanyika nchini.

Kupitia jukwaa hilo la kidijitali, watumiaji wataweza kugundua ujio wa matukio yanayowavutia, yakiwemo matamasha, mashindano ya michezo, mikutano ya kibiashara, makongamano ya kidini, maonesho na shughuli za kijamii, huku wakipata taarifa muhimu kuhusu maeneo na muda wa matukio hayo.

Programu hiyo, ambayo tayari inapatikana kwa watumiaji wa simu za Android kupitia Google Play Store na tovuti yake, imeanzishwa kukabiliana na changamoto ya kutawanyika kwa taarifa za uwepo wa matukio na shughuli katika majukwaa tofauti hali inayosababisha baadhi ya wananchi kukosa fursa za kushiriki shughuli hizo licha ya wao kuzihitaji.

Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa programu hiyo, Samwel Gisayi, Mkurugenzi wa Ubunifu wa Kampuni ya Empirical Communications, kampuni mwandaaji wa jukwaa hilo, alisema wazo la Kunani Tizii limetokana na kutambua kuwa nchini kuna shughuli za kijamii na matukio mengi yenye umuhimu wa kijamii na kiuchumi, lakini taarifa za uwepo wa matukio hayo hazipatikani kwa urahisi kwa walengwa.

"Tanzania haikosi matukio, bali kinachokosekana ni mfumo uliopangwa vizuri na unaofikika kwa urahisi utakaowawezesha watu kufahamu uwepo na ujio wa matukio hayo. Mkutano muhimu, tamasha au shughuli ya kijamii inaweza kufanyika bila kufahamika na watu ambao wangeweza kunufaika kwa kushiriki. Kunani Tizii imeanzishwa kutatua changamoto hiyo kwa kuwaunganisha waandaaji wa matukio na walengwa wao kupitia jukwaa moja," alisema Gisayi.

Alilifafanua kwamba lengo kuu la programu hiyo ni kuyatambulisha matukio hayo kwa walengwa na sio kuripoti yalivyofanyika jukumu alilosema linafanywa na vyombo vya habari.

Alisema programu hiyo imeundwa kuhudumia makundi tisa ya matukio ambayo ni burudani, michezo, shughuli za Serikali na masuala ya umma, biashara, dini, elimu, biashara na maonesho, shughuli za kijamii na maendeleo ya jamii, pamoja na utalii na utamaduni.

Alifafanua kuwa kupitia mfumo huo, mtumiaji ataweza kupata taarifa za uwepo wa matamasha ya muziki, mechi za mpira wa miguu, mikutano ya kibiashara, makongamano ya kidini, maonesho ya kilimo, shughuli za Serikali, kampeni za afya na matukio mengine kulingana na mahitaji na maeneo anayopendelea.

Kwa upande wa teknolojia, Gabriel Mlolwa, Mtaalamu Teknolojia ya Habari (IT) wa Kampuni ya Empirical Communications na mtengenezaji wa programu hiyo, alisema Kunani Tizii imeundwa kurahisisha utafutaji wa uwepo wa matukio na kuwawezesha watumiaji kupanga ushiriki wao kupitia vipengele mbalimbali.

Alisema programu hiyo ina makundi ya taarifa za matukio kama "Happening Today" (Matukio ya Leo), "This Weekend" (Matukio ya Mwishoni mwa Wiki), "Free Events" (Matukio ya Bure), "Popular Events" (Matukio Maarufu) na "Coming Soon" (Matukio Yajayo).

Aidha, ina kipengele cha "Near Me" kinacholenga kumwezesha mtumiaji kutambua matukio yanayofanyika karibu na eneo alipo, huku mfumo wa utafutaji ukimruhusu kuchagua matukio kulingana na maeneo na mambo anayopendelea.

"Katika utengenezaji wa programu hii, tulilenga kuhakikisha kuwa upatikanaji wa taarifa za uwepo wa matukio unakuwa rahisi. Mtumiaji hapaswi kulazimika kutembelea majukwaa mengi ili kupata taarifa za uwepo wa shughuli zinazomvutia. Kupitia vipengele kama utafutaji wa matukio kulingana na eneo, makundi ya matukio, kalenda na vikumbusho (reminders), tunarahisisha upatikanaji wa taarifa na maandalizi ya kushiriki," alisema Mlolwa.

Aliongeza kuwa watumiaji wanaweza kushiriki taarifa za matukio wanayoyapata kupitia WhatsApp, Instagram, Facebook, TikTok, X na barua pepe ili kuwawezesha watu wengine kupata taarifa hizo.

Mbali na kutoa taarifa kwa wananchi, programu hiyo pia inalenga kuwasaidia waandaaji wa matukio kutangaza shughuli zao na kuwafikia walengwa kwa urahisi zaidi.

Kwa mujibu wa Mlolwa akupitia kipengele cha Organiser Dashboard, taasisi na waandaaji wa matukio wataweza kufungua akaunti na kuchapisha taarifa kuhusu shughuli zao zikiwemo mabango, tarehe, maeneo ya kufanyika, wazungumzaji, wasanii, ratiba, taarifa za tiketi na viungo vya usajili.

Alisema mfumo huo utatoa fursa kwa vikundi vya kijamii, waandaaji wa matukio, taasisi za dini, taasisi za Serikali na kampuni binafsi kutangaza uwepo wa shughuli zao katika jukwaa moja, huku wafanyabiashara na makampuni wakipata nafasi ya kutangaza bidhaa na huduma zao.

Katika kurahisisha upatikanaji wa tiketi, Mlolwa alisema Kunani Tizii imeundwa kwa lengo la kuunganisha taarifa za matukio na mifumo iliyopo ya utoaji wa tiketi pamoja na watoa huduma za malipo nchini, ili watumiaji waweze kupata huduma za usajili na ununuzi wa tiketi kwa urahisi zaidi.

Alisema jukwaa hilo pia linatarajia kuanzisha Kunani Tizii Weekend, utaratibu wa kuandaa na kuchapisha orodha ya matukio 10 bora ya mwishoni mwa wiki kila Ijumaa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano.

Kwa mujibu wa Mlolwa kwasasa wanajipanga kuanzisha toleo la programu hiyo kwa watumiaji wa iOS, huku maboresho yajayo yakijumuisha mfumo wa tathmini na maoni kuhusu matukio na maeneo ya kufanyia shughuli mbalimbali.

Aliwahimiza Watanzania, wafanyabiashara, taasisi na waandaaji wa matukio kupakua programu hiyo kupitia Google Play Store, kutembelea tovuti yake na kufuatilia kurasa zake za mitandao ya kijamii pamoja na chaneli ya YouTube ili kupata taarifa za matukio na fursa mbalimbali zinazoendelea nchini.

“Tunalenga kuifanya Kunani Tizii kuwa jukwaa ambalo Watanzania watalitumia wanapohitaji kufahamu kinachoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ili kufanikisha hili tunawaomba sana waandaaji wa matukio waitumie program huu kusajili ujio wa matukio yao bila kutozwa gharama yoyote ili taarifa za uwepo wa matukio hayo ziwafikie walengwa wengi zaidi ’’ alihitimisha Mlolwa.
Mkurugenzi wa Ubunifu wa Kampuni ya Empirical Communications, Samwel Gisayi (aliesimama) akiwasilisha dhana ya utendaji kazi wa Program tumishi ya Kunani Tizii mbele ya wadau hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...