Bolt Tanzania, kampuni inayoongoza nchini katika huduma za usafiri mtandaoni, kwa kushirikiana na Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliandaa hafla na warsha iliyowakutanisha wanafunzi zaidi ya 300 kujifunza namna ya kutumia vipengele vya usalama katika programu ya Bolt, kuripoti matukio yanayohatarisha usalama na kuchangia safari salama.

Kupitia maonesho ya vitendo, maswali ya kupima uelewa wa usalama na mijadala iliyohusisha wawakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Polisi wa Usalama Barabarani na Bolt, wanafunzi walijifunza namna teknolojia inavyoweza kusaidia kutimiza wajibu wa kila siku katika matumizi salama ya barabara.

Wanafunzi walifahamishwa kuhusu vipengele vinane vya usalama vinavyotumika katika huduma za Bolt nchini Tanzania.

“Nimejifunza kuwa namba maalumu za uthibitisho wa safari, yaani Pickup Codes, husaidia kuhakikisha abiria anapanda gari sahihi, huku Driver Selfie Verification ikithibitisha utambulisho wa dereva kwa kutumia picha ya uso wake. 

Share Trip huwawezesha abiria na madereva kuwashirikisha wengine taarifa za safari inavyoendelea, wakati Ride Check hutambua gari linaposimama kwa muda mrefu usio wa kawaida na kutoa arifa za kuhakiki usalama,” alisema Masanja, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyehamia Dar es Salaam hivi karibuni.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Daimoni Mwakigowe, aliishukuru Bolt Tanzania kwa ushirikiano huo, akisema umefanyika wakati mwafaka ambapo muhula wa kwanza umeanza na maelfu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wamewasili kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwa na uhitaji wa kufahamishwa kuhusu maisha ya jijini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wanafunzi, Bi. Paulina Mabuge, aliyekuwapo katika hafla hiyo, alisema: “Matumizi ya Bolt yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wanafunzi wengi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Kadiri Tanzania inavyopanua matumizi ya teknolojia ya kidijitali, wanafunzi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuimudu, hasa katika mahitaji muhimu ya kila siku kama usafiri, ili kuimarisha usalama na ufanisi.”

Meneja wa Uendeshaji wa Bolt Tanzania, Ludwigy Bwana, alisema ushirikiano huo unalenga kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu usalama.

“Wanafunzi ni sehemu muhimu ya watumiaji wa Bolt, na ushirikiano huu unasaidia kuziba mapengo ya uelewa katika maeneo muhimu kama usalama. Uwekezaji wetu katika teknolojia unaenda sambamba na elimu ya vitendo inayowasaidia abiria na madereva kutambua hatari na namna ya kupata msaada. Vipengele vya usalama huwa na manufaa zaidi pale watu wanapojua kuvitumia.

“Vijana, ambao sehemu kubwa yao ni wanafunzi, ni zaidi ya asilimia 70 ya watu nchini Tanzania. Kwa kuwashirikisha wanafunzi, tunalenga kujenga mazoea ya kuzingatia usalama kila siku, ambayo yataenea kutoka chuoni hadi katika familia na jamii,” alisema Ludwigy.

Naye Pateli Ngereza, Kaimu Meneja wa Udhibiti wa Magari ya Usafiri wa Abiria na Mkuu wa LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, alisisitiza umuhimu wa abiria kudai huduma zinazozingatia kanuni.

“Abiria wana haki na wajibu wa kudai huduma zinazokidhi matakwa ya kisheria. Wataalamu na wanafunzi wana wajibu wa kutumia mifumo iliyopo, ikiwemo programu ya LATRA, kuchagua vyombo vya usafiri wa ardhini vyenye leseni, kutumia vifaa vya usalama kama kofia ngumu na mikanda ya usalama, pamoja na kuripoti vitendo vinavyohatarisha usalama,” alisema Ngereza.

Hafla hiyo iliwahimiza wanafunzi kuwashirikisha wenzao elimu waliyoipata na kuhakikisha safari za Bolt zinafanyika kupitia programu hiyo, ili waendelee kunufaika na vipengele vyake vya usalama na waweze kuripoti matukio yanapojitokeza.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...