Na Janeth Raphael - MichuziTv 

BENKI ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana (OR-MV) imesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuwawezesha vijana wa vyuo vikuu na vyuo vya kati kupitia majukwaa ya vijana yanayojulikana kama Campus Connect.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uendeshaji wa makongamano ya Campus Connect na kuwafikia vijana zaidi ya 300,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano, kwa kuwajengea uwezo katika maeneo ya ubunifu, ujasiriamali, biashara, vipaji pamoja na matumizi ya fursa mbalimbali za kiuchumi.

Hafla ya uwekaji saini wa makubaliano hayo imefanyika leo, Novemba 9, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, jijini Dodoma, ikiwa ni hatua inayodhihirisha dhamira ya CRDB katika kuchangia maendeleo na uwezeshaji wa vijana nchini.

Kupitia ushirikiano huo, vijana pia wataunganishwa na fursa za mitaji na masoko, hatua itakayowawezesha kubadilisha mawazo na bunifu zao kuwa biashara na shughuli zenye tija kwa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Bi. Jenifa Christian Omolo, amesema uwezeshaji wa vijana unapaswa kuanza mapema wanapokuwa vyuoni ili kuwajengea maarifa, uelewa na ujasiri wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.

Amesisitiza kuwa jukwaa la Campus Connect linapaswa kuwa mfumo endelevu wa kuwafuatilia na kuwaendeleza vijana kuanzia wanapokuwa vyuoni hadi wanapohitimu na kuanza maisha ya kujitegemea, ili kuhakikisha wanatumia ipasavyo maarifa na fursa wanazopatiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kutoka Benki ya CRDB amesema ushirikiano huo unaongeza nguvu katika kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kifedha mapema, kuwawezesha kubuni mawazo, kuanzisha biashara na kutumia kikamilifu fursa za kujiajiri. Amesema kupitia ushirikiano huo, CRDB itaendelea kuwa sehemu muhimu ya safari ya kuwaibua na kuwawezesha vijana, ili waweze kukuza shughuli zao za kiuchumi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...