NA DENIS MLOWE, IRINGA

MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Dk. Linda Selekwa, ametoa wito kwa madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kuimarisha juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu na kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa uhakika.

Dk. Selekwa alitoa wito huo wakati akitoa salamu za Serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ambapo alisisitiza kuwa madiwani wana nafasi kubwa ya kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kutokana na ukaribu wao na jamii.

Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kupitia mfumo wa bima, hivyo ni muhimu viongozi wa ngazi za chini kuelewa mfumo huo na kuwahamasisha wananchi kujiunga.

Alieleza kuwa wananchi wengi wamekuwa wakifika katika ofisi za viongozi kuomba msaada wa gharama za matibabu, wakati baadhi ya changamoto hizo zingeweza kupunguzwa kwa kuwa na bima ya afya inayowasaidia kugharamia matibabu kwa kipindi chote cha uanachama.

“Tunawaomba madiwani kutumia nafasi zenu kuhakikisha mnaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya. Mtu anapougua katika jamii, mara nyingi kiongozi wa kwanza anayemfuata ni diwani au mwenyekiti wa eneo husika, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu mfumo huu,” alisema.

Dk. Selekwa alisisitiza kuwa uhamasishaji huo unapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwemo miundombinu, vifaa na utayari wa watumishi ili wananchi wanapojiunga na bima wapate huduma zinazostahili.

Alionya kuwa endapo wananchi watahamasishwa kujiunga na bima lakini vituo vya afya vikakosa uwezo wa kutoa huduma kwa wakati, hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa na kupunguza imani yao kwa mfumo huo.

Aidha Dk. Selekwa aliipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kuendelea kuimarisha shughuli za maendeleo, hususan maonyesho ya biashara yaliyofanyika hivi karibuni ya biashara Mufindi.akisema yamekuwa na mchango katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kutangaza bidhaa na huduma zao.

Alisema maonyesho yamekuwa na matokeo chanya kutokana na ushirikiano wa Baraza la Madiwani na wataalamu wa halmashauri, huku akiwataka viongozi hao kuendelea kuyasimamia ili yawe endelevu na kuongezeka ukubwa kila mwaka.

Aliwasisitiza madiwani kuhakikisha maonyesho hayo yanakuwa sehemu ya utamaduni wa halmashauri, akieleza kuwa hata viongozi watakapobadilika, mipango na mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kuendelezwa.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alilitaka Baraza la Madiwani kusimamia kwa karibu mabadiliko ya kiutendaji yanayotokea katika halmashauri, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya madiwani, watumishi na viongozi wapya wanaopangiwa majukumu mbalimbali.

Alisema mabadiliko ya viongozi hayapaswi kuwa sababu ya kuyumba kwa utendaji wa halmashauri, bali yanapaswa kuwa fursa ya kuimarisha taasisi na kuendeleza misingi mizuri iliyowekwa na viongozi waliotangulia.

Aliongeza kuwa mafanikio yanayopatikana katika halmashauri yanapaswa kuonekana kama matokeo ya ushirikiano wa viongozi na watumishi wote, hivyo ni muhimu kulinda sifa na heshima ya taasisi hiyo kwa kuimarisha usimamizi na uwajibikaji.

Dk. Selekwa pia alitambua mchango wa aliyekuwa kiongozi wa halmashauri, Federica Myovela ambaye alisema ameacha msingi mzuri wa utendaji, huku akiwataka madiwani na watumishi kuendeleza ushirikiano na uongozi unaoendelea.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...