▪️ Aonya dhidi ya kujichukulia sheria mikononi na kuuza ardhi kinyemela
▪️ Serikali yakamilisha usanifu wa barabara ya njia sita kutoka Picha ya Ndege hadi Chalinze
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekemea tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuonya kuwa Serikali haiungi mkono uvunjaji wa sheria wa makusudi.
“Tusiruhusu uvunjifu wa sheria wa makusudi kwa sababu utaua udugu wetu uliokuwepo kwa miaka mingi. Lazima tuzingatie utawala wa sheria, tuache utaratibu wa uvunjifu wa sheria na kujichukulia sheria mkononi,” amesisitiza.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Polisi, wilayani Chalinze, mkoani Pwani, jana jioni (Jumamosi, Novemba 21, 2026), Waziri Mkuu alisema mmomonyoko wa utawala wa sheria unaalika visasi na makovu yasiyopona.
“Tusibaguane au kuchukiana kwa sababu ya ardhi kwani yenyewe haiongezeki lakini mahitaji ya ardhi yanaongezeka. Tunatakiwa tuweke nguvu kubwa katika kupanga matumizi bora ya ardhi na tuheshimu sheria,” alisisitiza.
Dkt. Mwigulu alisema Serikali haitavumilia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu vya kulisha mifugo kwenye mashamba ya watu wengine kwa makusudi, kujeruhi mifugo au kushambulia watu kwa kulipiza kisasi.
“Kama mifugo yako inapenda kula mazao ya mashambani, basi lima mashamba yako kisha uingize mifugo yako shambani mwako. Mambo ya kuchukua chukua sheria mkononi yanaalika visasi. Na damu ikimwagika katika ardhi inaleta laana,” alisema.
Aliwaagiza viongozi wa wilaya na vijiji washughulikie migogoro hiyo kwa mujibu wa sheria, huku akikemea uuzaji wa ardhi kinyemela na kusisitiza kuwa kosa la mtu mmoja halipaswi kugeuzwa kuwa kosa la jamii nzima.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema uchunguzi wa mgogoro wa mipaka kati ya vijiji vya Pingo na Chamakweza umekamilika na taarifa yake iko tayari kwa hatua zinazofuata.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka miradi mingi kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo, ikiwemo ya maji, elimu, afya na barabara.
“Wakati naanza ubunge, hatukuwa na Hospitali ya Wilaya lakini hivi sasa tumekamilisha ujenzi wake na tumepata shilingi bilioni tatu za ujenzi wa ICU,” alisema.
Alisema zamani, pakitokea ajali yoyote kati ya Kabuku (Tanga) na Chalinze (Pwani), walikuwa wakikimbilia Hospitali ya Tumbi ili kupeleka majeruhi huko, lakini kwa sasa hawatalazimika kuitegemea tena hospitali hiyo kwani wamepata kitengo cha wagonjwa wa dharura (EMD) cha kisasa kabisa.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, alisema vijiji hivyo ni miongoni mwa vijiji 16 vilivyopangwa kuandaliwa mipango bora ya matumizi ya ardhi mwaka huu ili kusaidia kutatua migogoro iliyodumu kwenye maeneo hayo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema Serikali imekamilisha usanifu wa barabara ya njia sita yenye urefu wa kilometa 74, kutoka Picha ya Ndege hadi Chalinze, inayotarajiwa kutekelezwa kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Alisema uthamini wa maeneo yanayohitajika kwa ajili ya mradi huo unaendelea, huku Serikali pia ikipanga kuboresha barabara iliyopo ya Dar es Salaam–Kibaha–Mlandizi–Chalinze ili kupunguza msongamano wa magari.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...