· Chazinduliwa na Jaji Mkuu Masaju
· Chaeleza historia na mchango wa Jaji Mstaafu Eusebia Nicholas Munuo
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Tarehe 17 Novemba, 2026 itabaki kuwa katika historia ya Mhimili wa Mahakama na Taifa la Tanzania kwa ujumla kufuatia tukio la uzinduzi wa Kitabu cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Nicholas Munuo aliyekuwa Mwanamke wa kwanza Mtanzania kuwa Hakimu na Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Katika kusherehekea mchango mkubwa wa Jaji Mstaafu huyo almaarufu kwa jina la Mama Munuo/Jaji Munuo, Mahakama ya Tanzania kupitia aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma iliona umuhimu wa kuwa na kitabu kitakachoeleza historia yake, hivyo, walikieleza Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuandika Kitabu cha Historia ya Mwanamama huyo mahiri kufuatia historia yake nzuri na utumishi wa umma uliotukuka kwa Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Wazo la kuandika kitabu hicho lililozaliwa tarehe 20 Machi, 2024 limezaa matunda na kuja na Kitabu kiitwacho ‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania,’ ambacho kimezinduliwa na Mgeni Rasmi wa hafla ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Kitabu hicho ni hazina mpya na dira muhimu ya kisheria na kimaadili kwa kizazi cha sasa na kijacho na kinasalia kuwa funzo kwa Majaji, Mahakimu, Wanasheria, Wanafunzi wa Sheria na kila Mtanzania kuwa mafanikio ya kweli hujengwa kwa maono, uwezo, ujasiri, nidhamu, uadilifu na moyo wa dhati wa kuitumikia jamii.
Akitoa hotuba yake kabla ya kuzindua Kitabu hicho, Mhe. Masaju amesema kuwa, uzinduzi wa kitabu hicho unadhihirisha kwa mara nyingine tena umahiri, ujasiri na alama isiyofutika iliyoachwa na Jaji Mstaafu, Mhe. Munuo katika utumishi wake uliotukuka uliodumu kwa miongo kadhaa, ukiwa ni kielelezo cha umahiri wa kipekee na utetezi thabiti wa misingi ya haki, usawa na utawala wa sheria nchini Tanzania.
Jaji Mkuu amekiri kufurahishwa na tukio hilo na kusema kuwa, kwake ni faraja na anamshukuru Mungu kwa kumpa fursa hiyo ya kuzindua kitabu hicho, ambapo amesema, “nina furaha kubwa kushiriki tukio hili lenye umuhimu mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania,Taaluma ya sheria, masuala ya jinsia na Taifa letu kwa ujumla, kwani leo hatuzindui kitabu tu, tunazindua kumbukumbu ya historia, tunatambua mchango wa mtumishi aliyejitolea maisha yake katika utumishi wa haki na tunahifadhi utetezi wa taaluma kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.”
Amesema, tukio hilo ni la uhusishaji wa maarifa, uhusishaji wa hekima na akili, lakini na maadili katika utumishi na jamii ya watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Mahakama itaendeleza matukio hayo ya uandishi wa vitabu kwa Majaji na watumishi wengine wa Mahakama waliostaafu, kama sehemu na mkakati wa kuhifadhi maarifa, Hekima, akili na maadili ya wenzetu.
Mhe. Masaju amesema kitabu hicho kitabu hicho kina umuhimu unaozidi maelezo ya maisha ya mtu mmoja na kwamba ni nyaraka ya kihistoria ya mageuzi ya Mahakama ya Tanzania; ni kumbukumbu ya juhudi za wanawake katika taaluma ya sheria; ni ushahidi wa mabadiliko ya nafasi ya mwanamke katika uongozi wa kitaifa na kimataifa; na zaidi ya yote, ni somo kuhusu namna mtu mmoja anavyoweza kuacha alama katika taasisi na jamii nzima.
“Kwa kusoma kitabu hiki, ndipo tunaweza kujua kujifunza mambo mengi yaliyofanywa na Mhe. Munuo alipokuwa katika utumishi wa umma katika Mhimili huu wa Mahakama,” ameeleza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju amesema kuwa, Jaji Eusebia Nicholas Munuo si sehemu tu ya historia ya Mahakama ya Tanzania bali ni miongoni mwa watu walioisaidia historia hiyo kubadilika katika Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia historia ya Jaji Munuo, Jaji Mkuu amesema, kuna haja ya kuangalia maisha yake si kwa kuhesabu tu vyeo alivyowahi kushika, bali kuangalia milango aliyofungua, taasisi alizojenga, watu aliowainua, kanuni za haki alizozisimamia na kizazi cha wataalam alichokipa ujasiri wa kuamini kwamba nacho kinaweza kufika mbali.
Aidha, Mhe. Masaju amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kulitekeleza jukumu la kuandika kitabu hicho kwa ufanisi ipasavyo mara tu walipoelekezwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wa wakati huo, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na wote walioshiriki kuandika na kuweka mada zao ndani ya kitabu hicho.
Ametoa rai kwa Uongozi wa Mahakama, bado kuna haja na deni kubwa la kuendelea kuandika vitabu kwa Majaji wengine na hasa ambao bado wako hai. Miongoni mwao ameshauri uangaliwe uwezekano wa kuandika mapema iwezekanavyo kitabu kinachohusu sifa za maisha ya Jaji Damian Lubuva.
Akizungumzia maisha na safari ya uongozi wa Mhe. Munuo, Jaji Mkuu amesema kwamba, ni kielelezo cha pekee cha uvumilivu, uwezo mkubwa, na utumishi uliotukuka uliovunja vizuizi vya kijinsia na kuweka msingi thabiti katika mfumo wa sheria na utoaji haki nchini Tanzania.
Amesema, safari ya Jaji Munuo ndani ya Mhimili wa Mahakama ni ushahidi thabiti kuwa, uwezo hauna jinsia. Alianza kazi yake akiwa na umri wa miaka 24 na kuvunja rekodi katika kila ngazi aliyopitia ambazo ni pamoja na kuwa Hakimu Mkazi wa Kwanza Mwanamke Tanzania aliajiriwa rasmi tarehe 01 Julai, 1970 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Dar es Salaam, Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Vituo vya Mwanza na Tabora, akiongoza shughuli za kimahakama, ugawaji wa mashauri, na usimamizi wa watumishi.
Nafasi nyingine alizowahi kushika Jaji Munuo ni pamoja na Hakimu Mkazi mwenye Mamlaka ya Ziada (1984), Jaji wa Mahakama Kuu (1987): alipandishwa cheo na kuhudumu katika kanda mbalimbali zikiwemo Mbeya, Songea, Moshi, na Dar es Salaam, Jaji wa Mahakama ya Rufani (2002), alikuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika Mahakama ya juu ya Nchi.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Jaji Munuo aliwahi pia kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania ambapo alikabidhiwa dhamana ya kuiongoza Mahakama nzima ya Tanzania katika vipindi mbalimbali.
Mbali na vyeo hivyo, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, Mhe. Munuo alienda zaidi ya hukumu na kuwa Mwalimu, Mlezi na Mjenzi wa Taasisi. Amesema, “Jaji Munuo hakuwa tu mtoa maamuzi ya kisheria, bali alikuwa mchango hai katika kujenga uwezo wa kitaaluma na taasisi imara nchini.”
Kwa upande wa Elimu na Mafunzo, Mhe. Masaju amesema kuwa, Jaji Munuo aliwahi kuwa Mhadhiri katika Chuo cha Usimamizi wa Maendeleo Mzumbe (IDM), akiandaa Maofisa Mahakama na Mahakimu. Alikuwa mtoa mada mkuu katika maadili ya Mahakama, haki za binadamu, usawa wa kijinsia, na kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono (sextortion).
Vilevile, Jaji Munuo alifanya Utumishi wa Kitaifa Nje ya Mahakama ambapo aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Regional Housing Tribunal, Arusha (1984 - 1987), Mwenyekiti wa Regional Local Government Election Committee, Kamishna wa Law Reform Commission of Tanzania (1984 - 1990), akishiriki katika uchunguzi wa mfumo wa haki jinai, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Majaji (2007–2012) na Mwenyekiti wa National Parole Board of Tanzania (2013–2016).
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amesema kuwa, ili kuhakikisha kuwa mafanikio yake hayabaki kuwa ya pekee yake, Jaji Munuo aliongoza juhudi za kuanzisha Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) mwaka 2000, akihudumu kama Mwanzilishi na Mwenyekiti wake wa kwanza ili kuwajengea uwezo, kuwaunganisha, na kuwalinda wanawake na watoto kisheria.
“Ushawishi wake ulivuka mipaka ya nchi hadi kufikia kuongoza International Association of Women Judges (IAWJ) kama Rais wa Kimataifa (2012 - 2014). Chini ya uongozi wake, Tanzania iliweka historia ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Kimataifa wa IAWJ uliofanyika Arusha mwezi Mei, 2014,” amesema Mhe. Masaju.
Kwa upande wa Maamuzi muhimu ya Kimahakama yaliyounda Sheria, Jaji Mkuu amesema kupitia maamuzi yake makuu ya kimahakama, Jaji Munuo alisaidia kuimarisha misingi ya kisheria na utawala bora nchini.
Mhe. Masaju amesema mchango wa Jaji Munuo ulitambuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Desemba, 2012 alipotunukiwa nishani ya heshima ya kitaifa ya Nishani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daraja la Pili (Order of the United Republic of Tanzania, Second Class Medal) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na tuzo nyingine za kitaifa na kimataifa.
Mhe. Eusebia Munuo alizaliwa tarehe 01 Septemba, 21946 katika Kijiji cha Njari, Uru Kaskazini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Hafla ya uzinduzi wa Kitabu hicho iliyoratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto imehudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani, baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama na ya IJA pamoja na Watumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizindua Kitabu cha historia ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Nicholas Munuo kinachoitwa ‘JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania’ tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania-Dodoma. Wanaoshuhudia zoezi hilo kushoto ni, Jaji Mstaafu, Mhe. Munuo na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimkabidhi Jaji Munuo nakala za vitabu vya JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania mara baada ya kukizindua tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Histioria ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Munuo kinachoitwa JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira na katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.



Majaji, Viongozi pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama Dodoma wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Histioria ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Munuo kinachoitwa JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati). Wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira, wa tatu kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Munuo, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eusebia Munuo akizungumza wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Kitabu chake kiitwacho JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania iliyofanyika tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa neno wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Kitabu chake kiitwacho JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania iliyofanyika tarehe 17 Novemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira akitoa neno tarehe 17 Novemba, 2026 wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Kitabu chake kiitwacho JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wakili Eric Ng'maryo akitoa maelezo kuhusu Mtazamo wa Kisheria katika Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Prof. Ruth Meena akitoa neno kuhusu Mtazamo wa Kijinsia katika Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama Dodoma waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Ndugu wa Jaji Mstaafu, Mhe. Eusebia Munuo (wa tatu kushoto).
Picha ya pamoja na sehemu ya walioshiriki kuandika Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Picha ya pamoja na Naibu Wasajili waliohudhuria katika uzinduzi wa Kitabu kijulikanacho kwa jina la JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) pamoja na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Picha ya pamoja na Mahakimu waliohudhuria katika uzinduzi wa Kitabu kijulikanacho kwa jina la JUSTICE EUSEBIA MUNUO: A Trailblazer In The Legal Profession in Tanzania kilichozinduliwa tarehe 17 Novemba, 2026 na Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
(Picha na JAMES BUSANYA & PAUL MAKANILE, Mahakama-Dodoma)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...