Na Victor Masangu, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, ametoa viti 100 na Sh milioni moja kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kata ya Viziwaziwa, kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowawezesha vijana kujipatia kipato.
Katika msaada huo, Sh milioni moja zitatumika kuanzisha mradi wa maegesho ya pikipiki (bodaboda), huku viti 100 vikiwa sehemu ya mradi mwingine wa kuwawezesha vijana kuongeza kipato.
Koka ametoa msaada huo wakati wa kikao cha Baraza la UVCCM Kata ya Viziwaziwa, ambapo pia alifungua rasmi Shina la Umoja wa Vijana wa Bodaboda Mkomgeni na kuwataka vijana kuwa na mshikamano katika kusimamia na kuendeleza miradi yao.
Amewasisitiza vijana hao kuzingatia nidhamu ya fedha, usimamizi mzuri wa miradi na uwajibikaji ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na kuleta manufaa kwa wanachama.
“Kitu kikubwa ninachowaomba vijana wa UVCCM Kata ya Viziwaziwa ni kuendelea kushikamana pamoja na kuwa na nidhamu katika suala zima la utunzaji wa fedha, sambamba na kuhakikisha miradi waliyoianzisha inakuwa na tija,” amesema Koka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Viziwaziwa, Jumanne Mwagiya, amempongeza Mbunge huyo kwa kuwashika mkono vijana kupitia msaada wa fedha na viti, akisema utawasaidia katika jitihada za kujikwamua kiuchumi.
Naye Diwani wa Kata ya Viziwaziwa, Mohamed Chamba, amesema juhudi zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mbunge Koka, zimechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Baadhi ya vijana walioshiriki kikao hicho wamemshukuru Mbunge huyo kwa msaada huo, wakieleza kuwa miradi ya maegesho ya pikipiki na viti 100 itakuwa sehemu ya fursa za kujiongezea kipato.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...