Teknolojia ya kutumia miamba ya mawe Volca grow, kutengeneza mbolea inayosaidia kurejesha rutuba ya udongo na kuimarisha ukuaji wa mimea imetengenezwa na Kampuni ya McDonald Horticulture and Soil Specialist Ltd, ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya pembejeo zinazozingatia misingi ya kilimo ikolojia hai na utunzaji wa mazingira.

Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Naima Donald Mwakamele, amesema mbolea ya Volca Grow hutengenezwa kwa kusaga miamba ya mawe hadi kupata unga laini, kisha kuchanganywa na virutubisho vingine ili kupata bidhaa inayoweza kuchanganywa na maji na kutumika katika mashamba ya mazao mbalimbali.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo cha Mbogamboga, Maua na Matunda Afrika (Hortilogistical Africa 2026) yanayofanyika mkoani Arusha, Mwakamele amesema teknolojia hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa mizizi ya mimea ili iweze kufyonza virutubisho na kuvisambaza katika sehemu mbalimbali za mmea, huku madini ya calcium yaliyomo yakisaidia kuimarisha mashina na kuweka uwiano wa asidi katika udongo.

Amesema mbolea hiyo inaweza kutumika katika mazao mbalimbali yakiwemo kahawa, karafuu, maua na mbogamboga, huku mchango wake katika kuboresha udongo ukiweza kudumu hadi miaka minne, jambo linaloweza kuwasaidia wakulima kuimarisha afya ya udongo kwa muda mrefu.

Akielezea chimbuko la teknolojia hiyo, Mwakamele amesema wazo la kutengeneza bidhaa hiyo lilianza miaka kadhaa iliyopita katika, ambapo walifanya majaribio katika Jangwa la Kalahari nchini Namibia, ambako kampuni ilifanya majaribio ya kutumia miamba ya mawe katika mazingira magumu ya kilimo na kufanikiwa kustawisha mimea ya nyanya, hatua iliyowahamasisha kuendeleza teknolojia hiyo na kuona namna inavyoweza kuwanufaisha Watanzania.

Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma kutoka Songwe na Mbeya kwenda maeneo mengine nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, akibainisha kuwa wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro na zabibu mkoani Dodoma ni miongoni mwa makundi yanayoweza kunufaika na matumizi ya mbolea hiyo.

Kwa upande wake, Paul Chilewa kutoka Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), ambao ni  mwamvuli unaohamasisha maendeleo ya kilimo ikolojia hai nchini, amesema matumizi ya pembejeo hai ni muhimu katika kulinda rutuba ya udongo, afya za wakulima na walaji pamoja na kuimarisha uzalishaji endelevu wa mazao.

Amesema Mkakati wa Kilimo Ikolojia Hai wa Wizara ya Kilimo unasisitiza umuhimu wa upatikanaji wa pembejeo zinazozingatia mazingira na kusaidia kuendeleza mifumo endelevu ya kilimo, hivyo ni muhimu kuendelea kuhamasisha ubunifu wa teknolojia zinazochangia kuboresha afya ya udongo na kuongeza tija katika uzalishaji.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...