Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), CPA Ahmed Kitara, amewataka wajasiriamali wanufaika wa mradi wa tuinuke pamoja kuendelea kuboresha bidhaa zao kwa kuzingatia ubora, vifungashio na mahitaji ya soko ili kuongeza ushindani na kupata fursa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo Novemba 3, 2026 jijini Dodoma, mara baada ya kutembelea banda la wanufaika wa Mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na Shirika la Aga Khan Foundation katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, katika Maonesho ya Viwanda na Biashara yanayoelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda na Sera ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2025, utakaofanyika Novemba 4, 2026.

Amesema bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali waliopatiwa mafunzo na SIDO zimeonesha kukidhi viwango na kuwa na uwezo wa kushindana katika masoko mbalimbali, akibainisha kuwa baadhi ya bidhaa hizo zimezalishwa na vijana, hususan wanawake, aidha, amewashauri wajasiriamali kujisajili na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kupata uthibitisho wa ubora na nembo ya Made in Tanzania itakayoongeza ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya nje.

Amesema SIDO iko tayari kuwawezesha wajasiriamali kupitia maeneo manne ambayo ni mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji, teknolojia rahisi za uzalishaji, huduma za mitaji pamoja na upatikanaji wa maeneo ya kufanyia kazi. Amewahimiza vijana na wajasiriamali kutumia fursa hizo kuanzisha biashara na kuzalisha bidhaa zenye ubora zinazokidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza Mnufaika wa mradi wa Tuinuke Pamoja, Keto khalfan kutoka Kata ya Chang'ombe Wilaya ya Dodoma, amesema maelekezo waliyopewa kuhusu ubora, ufungashaji na usajili wa bidhaa itawasaidia kuboresha bidhaa zao na kupanua masoko, ambapo kwa sasa bidhaa zao zinauzwa zaidi ndani ya mkoa na mikoa jirani huku akieleza kuwa SIDO imekuwa msaada kwao kupitia mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji, usimamizi wa fedha, ufungashaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Haruna Makunda, mnufaika wa mradi huo kutoka kikundi cha Kondoa Women Group, Wilaya ya Kondoa, amesema ushiriki wao katika Maonesho ya Viwanda na Biashara umewawezesha kupata elimu kuhusu umuhimu wa kusajili biashara kupitia BRELA na kupata uthibitisho wa ubora kutoka TBS ili bidhaa zao ziweze kuingia katika masoko mapana zaidi ikiwemo ya kimataifa, pia kuboresha vifungashio na ubora wa bidhaa ili kukidhi mahitaji ya soko la kisasa, huku akieleza kuwa maelekezo waliyopata kutoka SIDO yatawasaidia kuendeleza biashara zao.

Mjasiriamali kutoka kikundi cha Girls Power, Esther Kakurwa Wilaya ya Chamwino, amelipongeza Shirika la Aga Khan Foundation kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja, kwa kushirikisha wajasiriamali katika maonesho hayo akisema fursa hiyo imewasaidia kujitangaza, kujifunza na kupata uelewa wa namna ya kukuza biashara zao, huku akiwahimiza wajasiriamali wengine kuendelea kushiriki maonesho ili kupanua fursa za kibiashara.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...