Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kampuni ya bima ya Sanlam Allianz zimesisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano katika kupanua wigo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima nchini kupitia mfumo wa utoaji wa huduma za bima kupitia benki (Bancassurance), kwa lengo la kukuza ujumuishi wa kifedha na kuwawezesha wananchi kupata kinga dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuathiri afya, maisha na mali zao.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza elimu kwa wananchi, kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima na kuimarisha uwazi pamoja na ufanisi katika kushughulikia madai ili kujenga imani na kuongeza matumizi ya bima nchini.Dhamira wa wadau hao imebainishwa katika semina mtandao ya pili iliyoandaliwa na NBC kwa ushirikiano na Sanlam Allianz, yenye mada “Building Trust Through Transparency in Insurance” (Kujenga Imani Kupitia Uwazi Katika Huduma za Bima), iliyowakutanisha pia wawakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na DigiCash.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Bima wa NBC, Benjamin Nkaka, amesema benki zina nafasi muhimu katika kuwafikishia wananchi huduma za kinga ya kifedha kupitia bima, kwa kutumia mtandao wa matawi, wateja na mifumo ya kidijitali.
“Ushirikiano wetu na Sanlam Allianz umekuwa muhimu katika kupanua upatikanaji wa huduma za bima nchini. Kupitia mtandao wetu, tunawezesha upatikanaji wa bidhaa za bima, malipo ya ada za bima, elimu na mikopo ya kugharamia huduma hizo,” amesema Nkaka.
Alisisitiza kuwa bima haipaswi kuonekana kama huduma ya anasa, bali nyenzo muhimu ya usalama wa kifedha kwa kila mwananchi.
Kwa upande wake, Meneja wa Usambazaji wa Bidhaa za Bima wa Sanlam Allianz, Geofray Masige, alisema ushirikiano huo unawawezesha wateja kupata huduma za kibenki, mikopo, bima na msaada wa kushughulikia madai kupitia kituo kimoja.
“Ushirikiano huu unaunganisha huduma za benki na bima ili kumrahisishia mteja kupata suluhisho mbalimbali za kifedha sehemu moja,” alisema Masige.
Aliongeza kuwa kupitia ‘Insurance Premium Financing’, wateja wanaweza kugharamia ada za bima mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo kwa njia ya mikopo kutoka benki na kurejesha fedha kwa awamu, badala ya kulipa gharama zote kwa mkupuo.
Akizungumzia usimamizi wa sekta hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Uzingatiaji na Tathmini wa TIRA, Alex Rocky, alisema ushirikiano kati ya mamlaka, benki na kampuni za bima ni muhimu katika kuongeza elimu na kulinda haki za watumiaji.
“Ukuaji wa soko la bima unapaswa kwenda sambamba na uwazi na ufanisi katika kushughulikia madai ya wateja. Ni muhimu madai yanayostahili kulipwa kwa wakati ili kuimarisha imani ya wananchi,” alisema Rocky.
Alieleza kuwa taarifa ya utendaji wa soko la bima kwa mwaka 2025 imeonesha ongezeko la thamani ya ada za bima kutoka Sh trilioni 1.52 hadi Sh trilioni 2.25. Katika mwaka huo, kampuni za bima zililipa asilimia 80.8 ya madai yaliyopokelewa, yenye thamani ya takribani Sh trilioni 1.6, huku malipo yakifikia Sh trilioni 1.29.
Naye Dkt. Alfred Msemo kutoka DigiCash alisema uwazi katika utoaji wa huduma ni msingi wa kujenga uaminifu na kuongeza matumizi ya bima.
“Kampuni za bima zinapaswa kutumia lugha rahisi kueleza bidhaa, masharti ya mikataba na taratibu za madai ili wateja waelewe haki na wajibu wao,” amesema Dkt. Msemo, akisisitiza pia umuhimu wa teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Akizungumza kuhusu elimu kwa umma, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Masuala ya Udhibiti wa NBC, Sarah Laizer Sumaye, alisema baadhi ya wananchi bado wanaichukulia bima kama huduma inayotakiwa kisheria pekee badala ya kutambua manufaa yake katika kuwalinda dhidi ya hasara za kifedha, mali na afya.
“Tunatambua kuwa elimu ni muhimu katika kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu bima. Kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, NBC inaendelea kutoa elimu ya kifedha ili wananchi waelewe aina za bima, manufaa yake na umuhimu wake katika maisha yao,” alisema Sarah.
Alisisitiza kuwa elimu na ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kujenga utamaduni wa matumizi ya bima nchini
Meneja wa Usambazaji wa Bidhaa za Bima wa Sanlam Allianz, Geofray Masige (aliyeshika kipaza sauti), akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum yenye mada “Building Trust Through Transparency in Insurance” (Kujenga Imani Kupitia Uwazi katika Huduma za Bima), iliyoandaliwa na Sanlam Allianz kwa kushirikiana na Benki ya NBC, kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya maisha.
Waliokaa meza kuu kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Uzingatiaji na Tathmini wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Alex Rocky; Meneja Mkuu (Tathmini) wa Sanlam Allianz Life Insurance, Bi. Mary Murya; Mkuu wa Kitengo cha Bima wa NBC, Benjamin Nkaka; na Mtathmini kutoka kampuni ya DigiCash, Dkt. Alfred Msemo.
Mkurugenzi wa Huduma za Uzingatiaji na Tathmini wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Alex Rocky (katikati), akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum yenye mada “Building Trust Through Transparency in Insurance” (Kujenga Imani Kupitia Uwazi katika Huduma za Bima), iliyoandaliwa na Sanlam Allianz kwa kushirikiana na Benki ya NBC, kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya maisha. Kulia ni Meneja Mkuu (Tathmini) wa Sanlam Allianz Life Insurance, Bi. Mary Murya na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Biashara NBC na Muendesha mjadala huo Ibrahim Nzutu.
Meneja Mkuu (Tathmini) wa Sanlam Allianz Life Insurance, Bi. Mary Murya (katikati) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum yenye mada “Building Trust Through Transparency in Insurance” (Kujenga Imani Kupitia Uwazi katika Huduma za Bima), iliyoandaliwa na Sanlam Allianz kwa kushirikiana na Benki ya NBC, kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya maisha. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Bima wa NBC, Benjamin Nkaka na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Uzingatiaji na Tathmini wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Alex Rocky
Mtathmini kutoka kampuni ya DigiCash, Dkt. Alfred Msemo (Kulia) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum yenye mada “Building Trust Through Transparency in Insurance” (Kujenga Imani Kupitia Uwazi katika Huduma za Bima), iliyoandaliwa na Sanlam Allianz kwa kushirikiana na Benki ya NBC, kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya maisha. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Bima wa NBC, Benjamin Nkaka na katikati ni Meneja wa Usambazaji wa Bidhaa za Bima wa Sanlam Allianz, Geofray Masige
Akizungumza kuhusu elimu kwa umma, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Masuala ya Udhibiti wa NBC, Sarah Laizer Sumaye (Alieshika kipaza) alisema baadhi ya wananchi bado wanaichukulia bima kama huduma inayotakiwa kisheria pekee badala ya kutambua manufaa yake katika kuwalinda dhidi ya hasara za kifedha, mali na afya.

Baadhi ya washiriki wa semina mtandao (webnar) hiyo wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa tikio hilo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...