Wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri wamevutiwa na maajabu ya Hifadhi ya Ngorongoro baada ya kutembelea hifadhi hiyo na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na urithi wake wa kihistoria na kiutamaduni.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile, wahariri hao walipata maelezo kuhusu ushahidi wa kisayansi unaothibitisha uwepo wa binadamu wa kale katika Bonde la Olduvai, pamoja na simulizi ya mchanga unaohama maarufu kama mchanga wa mahaba.
Akizungumza na wahariri hao, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Abdul-Razaq Badru, amesema hifadhi hiyo ina mvuto wa kipekee kutokana na utajiri wa vivutio vya utalii na urithi wa utamaduni.
Amesema kuelekea Mashindano ya AFCON 2027, Ngorongoro imejipanga kupokea wageni kwa kuboresha miundombinu na huduma za utalii, ikiwemo mifumo ya malipo na ujenzi wa barabara yenye tabaka gumu kutoka Lango la Loduare hadi Seneto yenye urefu wa kilomita 29.5.
Aidha, amesema maboresho yanafanyika katika kivutio cha Maporomoko ya Maji ya Endoro, yakihusisha ujenzi wa ofisi za kisasa za kutolea huduma na njia za watembea kwa miguu.
Kwa upande wake, Balile amesema Ngorongoro ni mdau muhimu katika kuchangia pato la taifa na kuboresha huduma kwa wananchi kupitia mapato ya utalii, akiahidi kuwa Jukwaa la Wahariri litaendelea kutoa ushauri na kushirikiana kwa karibu na mamlaka hiyo katika kuendeleza hifadhi.



.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...