Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kuboresha afya za wananchi, uchumi wa familia, mazingira na maendeleo endelevu ya Taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema hayo leo Novemba 13,2026 wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, wenye kaulimbiu “Nishati Safi ya Kupikia kwa Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa 2050.”
Amesema mkutano huo una umuhimu kwa kuwa umewakutanisha waandishi wa habari, wataalamu, taasisi za Serikali na wadau wa sekta binafsi kujadili suala linalogusa maisha ya wananchi.
Amepongeza Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DAR-PC) kwa kuandaa mkutano huo na kuibua mjadala kuhusu nishati safi ya kupikia.
Kipangula amesema mafanikio ya matumizi ya nishati safi hayategemei uwepo wa teknolojia pekee, bali pia uwezo wa wananchi kumudu gharama na kupata huduma kwa urahisi.
Amesema familia zinazotaka kutumia gesi au umeme zinahitaji taarifa kuhusu gharama, usalama wa vifaa, upatikanaji wa huduma na namna ya kuendelea kuzitumia.
Amesema Serikali imeweka Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kufikisha matumizi hayo kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.
Ameeleza kuwa hatua zinazochukuliwa sasa ndizo zitakazosaidia kufikia malengo ya muda mrefu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Aidha, amesema matumizi ya nishati safi yanaweza kusaidia kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, hususan kwa wanawake na watoto wanaotumia muda mwingi katika maeneo ya kupikia.
Amesema nishati hiyo pia inaweza kupunguza muda unaotumika kutafuta kuni, kuhifadhi mazingira na kupunguza utegemezi wa rasilimali za misitu.
Kwa mujibu wa Kipangula, utekelezaji wa ajenda hiyo unaweza pia kufungua fursa za kiuchumi kupitia biashara ya vifaa, usambazaji wa nishati, huduma za ufundi, teknolojia na ubunifu.
Amesisitiza kuwa nishati safi ya kupikia si suala la kubadilisha aina ya jiko pekee, bali ni sehemu ya kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari, Kipangula amesema waandishi wana wajibu mkubwa wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu, gharama, usalama na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.
Amesema taarifa zinazotolewa zinapaswa kutumia lugha rahisi na kujikita katika mazingira halisi ya wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi.
Ameitaka media pia kuwapa wananchi nafasi ya kueleza uzoefu wao kuhusu matumizi ya nishati safi, pamoja na changamoto wanazokutana nazo.
Amesema taarifa hizo zinaweza kusaidia Serikali na wadau kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa programu mbalimbali.
Kipangula amewataka waandishi wa habari kuzingatia usahihi wa takwimu, ukweli na maadili ya taaluma wakati wa kuripoti masuala ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kasi ya usambazaji wa taarifa kupitia redio, televisheni, magazeti na majukwaa ya kidijitali isitumike kama sababu ya kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Amesema mwandishi mwenye weledi si anayewahi kutoa taarifa pekee, bali anayehakikisha taarifa hiyo ni sahihi, imehakikiwa na ina manufaa kwa jamii.
Ameitaka pia media kufuatilia utekelezaji wa miradi ya nishati safi na kuibua matokeo halisi kwa wananchi.
Kuhusu Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Kipangula amesema JAB inaendelea kusisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu kwa waandishi ili kuongeza weledi katika kuripoti masuala ya maendeleo ya Taifa.
Amesema sekta ya nishati inahitaji waandishi wenye uelewa wa sera, teknolojia, takwimu, uchumi na mazingira ili waweze kuuliza maswali sahihi na kuchambua taarifa za kitaalamu.
Ameitaka DAR-PC na taasisi zinazoshiriki katika mkutano huo kuangalia uwezekano wa kuanzisha au kuimarisha mafunzo kwa waandishi kuhusu nishati safi ya kupikia.
Amesema JAB iko tayari kushirikiana na wadau katika kujenga uwezo wa kitaaluma wa waandishi kwa mujibu wa majukumu yake ya kisheria.
Pia, Kipangula amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia inahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali, ikiwamo TTCL, TPA na BRELA, pamoja na sekta binafsi na wadau wengine.
Amesema TTCL inaweza kusaidia katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na mawasiliano kufikisha taarifa kuhusu bidhaa, huduma, bei na maeneo ya upatikanaji wa nishati safi.
Ameeleza kuwa TPA inaweza kuchangia katika kurahisisha usafirishaji wa vifaa vinavyohusiana na nishati hiyo, huku BRELA ikisaidia urasimishaji wa biashara na kufungua fursa kwa wajasiriamali.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati safi na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Kipangula amesema mafanikio ya mkutano huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya washiriki au mada zilizowasilishwa, bali kwa utekelezaji wa mapendekezo yatakayopitishwa.
Ametoa wito kwa vyombo vya habari kuandaa habari za kina kuhusu changamoto za wananchi katika matumizi ya nishati safi, ikiwamo gharama, usalama, usambazaji na fursa za biashara.
Amesema habari hizo zinaweza pia kushindanishwa katika tuzo mbalimbali za uandishi wa habari kama Samia Kalam Awards na EJAT, ili kuongeza ubora wa uandishi kuhusu masuala ya maendeleo.
Hatimaye, ametangaza rasmi kufunguliwa kwa Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...