Na Janeth Raphael MichuziTV Bungeni


Serikali imeweka mpango wa kuwawezesha wahitimu 10,000 wa vyuo vikuu na vyuo vya kati kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi (Internship) kila mwaka, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

Mpango huo unatekelezwa kupitia Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa Wahitimu, inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Akijibu swali la Mbunge wa Mwanakwerekwe, Kassim Hassan Haji, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwasaidia vijana wanaomaliza vyuo kupata nafasi za mafunzo ya vitendo ili kujenga uzoefu wa kazi, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Wilbard Munisi, amesema Serikali imekuwa ikitekeleza programu hiyo tangu mwaka wa fedha 2017/18.

Amesema katika kuhakikisha programu hiyo inakuwa na mwongozo unaoeleweka kwa wadau wote, Serikali iliandaa Mwongozo wa Taifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu wa mwaka 2017, unaotumika katika sekta ya umma na binafsi.

Dkt. Munisi amebainisha kuwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa programu hiyo mwaka 2017/18 hadi Septemba 2026, jumla ya wahitimu 34,549 wamepata fursa za mafunzo ya uzoefu wa kazi kupitia ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali.

Amesema kati ya wahitimu hao, 11,263 wamefanikiwa kupata ajira baada ya kukamilisha mafunzo yao, huku wengine 5,116 wakitumia ujuzi walioupata kuanzisha shughuli za kujiajiri.

Aidha, amesema Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa Wahitimu wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31, unaolenga kuongeza idadi ya vijana watakaonufaika na mafunzo hayo hadi wahitimu 10,000 kila mwaka.

Ameeleza kuwa mpango huo pia unalenga kupunguza pengo kati ya ujuzi unaopatikana katika taasisi za elimu na mafunzo na mahitaji halisi ya waajiri katika soko la ajira, ili kuwawezesha vijana kuwa na uwezo zaidi wa kupata ajira au kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...