Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekabidhiwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka Mtwara mjini hadi Tandahimba, mkoani Mtwara, wenye urefu wa kilomita 92.3.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Abdul Mihambo, amesema mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Wilaya za Tandahimba na Nanyamba.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya umeme na kuboresha huduma kwa wananchi, huku TANESCO ikishirikiana na ETDCO kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Mihambo ameyasema hayo wakati wa ziara ya kuitambulisha ETDCO kwa viongozi wa Wilaya za Tandahimba na Nanyamba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, huku kazi za awali zikianza kwa kusimika nguzo za umeme. Ameeleza kuwa kutokana na kasi ya utekelezaji, kampuni hiyo inalenga kukamilisha mradi kabla ya muda uliopangwa na kuomba ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kufanikisha kazi hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mtinjele, ameishukuru Serikali kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo, akisema utasaidia kuimarisha huduma ya umeme wilayani humo.
Wabunge wa Majimbo ya Nanyamba, Abdallah Chikota, na Tandahimba wameahidi kushirikiana na ETDCO kuhakikisha changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa mradi huo zinapatiwa ufumbuzi.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...