NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Kiwanda cha ASAS Dairies, akisema umechangia kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji na uchakataji wa maziwa mkoani Iringa na nchini kwa ujumla, sambamba na kupanua wigo wa fursa za ajira, hususan kwa vijana na wanawake.

Naibu Waziri Dkt. Pius Chaya ameyasema hayo leo, wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Iringa, ambapo ametembelea Kiwanda cha ASAS Dairies kilichopo mjini Iringa kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kutathmini mchango wa kiwanda hicho katika kukuza sekta ya maziwa nchini.

Ziara ya Naibu Waziri huyo mkoani Iringa inalenga kutathmini na kukagua hali ya uwekezaji, kubaini fursa zilizopo pamoja na changamoto zinazowakabili wawekezaji ili kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mkoani humo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Chaya ametembelea Kiwanda cha ASAS Dairies, kinachojihusisha na uchakataji wa maziwa, ambapo amepata fursa ya kujionea shughuli za uzalishaji, uwezo wa kiwanda pamoja na mchango wake katika kukuza uchumi kupitia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kutoa ajira kwa wananchi.

Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kutambua mahitaji ya wawekezaji na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea uwekezaji katika sekta mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji, ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye mmoja wa wakurugenzi wa Kiwanda cha ASAS Dairies, Ahmed Asas, amesema kuwa wao kama sehemu ya wadau muhimu katika sekta binafsi, wana wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, hususan kufanikisha malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Kiwanda cha ASAS Dairies kimetoa ajira kwa zaidi ya watu 400, ambapo asilimia 60 ya wafanyakazi hao ni wanawake, hatua inayochangia kuwawezesha kiuchumi wanawake pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...