Serikali imetenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi kupitia mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji na huduma, hatua inayolenga kukuza ujasiriamali, kuongeza ajira na kupanua ushiriki wao katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza Novemba 20, 2026, katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Kampasi Kuu Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula (Mb.), aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, amesema Serikali imeimarisha uwezeshaji huo kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kuanzisha Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi.
Amesema programu hiyo inalenga kuwapatia vijana mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi katika sekta mbalimbali, huku akiwataka wahitimu kutumia elimu na ujuzi walioupata kubuni biashara zenye tija zinazotatua changamoto za jamii na kukidhi mahitaji ya soko.
Aidha, amewataka vijana kuunda au kujiunga na vikundi vinavyokidhi vigezo, kujisajili katika mifumo ya manunuzi ya umma ikiwemo Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NeST), pamoja na kujifunza namna ya kuandaa na kuwasilisha zabuni ili kunufaika na fursa za Serikali.
Luswetula amesema Serikali imezielekeza taasisi zote za umma kuhakikisha makundi maalum, yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, yanapata angalau asilimia 30 ya thamani ya manunuzi yote ya bidhaa, huduma na kazi zinazohitajika kwa mwaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya, amesema chuo kitaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma na binafsi pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa katika kutekeleza miradi ya kimkakati na kutoa huduma za ushauri elekezi kwa ufanisi na weledi.
Amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa na chuo hicho kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania ni mradi wa kuimarisha ufuatiliaji na usalama wa shughuli za baharini katika maji ya pwani ya Tanzania, unaozingatia athari za mgogoro wa Bahari ya Shamu.
Ameeleza kuwa kupitia mradi huo, chuo kimevijengea uwezo zaidi ya vikundi 20 vya wananchi, hususan wanawake na vijana, katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, kuhusu shughuli za kilimo cha mwani.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la chuo hicho, Prof. Joseph Kuzilwa, amewataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kutatua changamoto za jamii, kuchochea ubunifu na kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya Taifa.
Amesema wahitimu wanapaswa kuwa wataalamu wenye weledi, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo, huku wakitumia changamoto kama fursa za kujifunza, kubuni suluhisho na kujiletea maendeleo kupitia ajira au kujiajiri.
Katika mahafali hayo, chuo kimewatunuku jumla ya wahitimu 6,076, wakiwemo wanaume 2,741 na wanawake 3,335.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...