Na Jane Mwakyoma

Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Rukwa limeiomba Serikali kutoa elimu ya lugha ya alama kwa watumishi wa taasisi za umma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Ombi hilo limetolewa katika kikao cha kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ustawi na maendeleo ya watu wenye ulemavu kilichofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo wameeleza kukumbana na changamoto ya mawasiliano wanapohitaji huduma katika ofisi za Serikali.

Wamesema changamoto hiyo imekuwa ikikwamisha upatikanaji wa huduma na utatuzi wa matatizo yao kutokana na baadhi ya watumishi kutokuwa na uelewa wa lugha ya alama.

“Tunapokwenda ofisini tukiwa na shida, kwa mfano mimi ni mlemavu wa kutokusikia, suala la kupata huduma linakuwa gumu kutokana na mtumishi kutokujua namna ya kunielewesha. Hali hii inatuletea ukakasi,” walisema.

Aidha, wameiomba Serikali kuhakikisha katika ofisi za umma, hususan ofisi za wakurugenzi wa halmashauri, kunakuwa na angalau mtumishi mmoja anayefahamu lugha ya alama ili kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kusikia kupata huduma na kuelewa maelekezo kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Mkoa wa Rukwa, Elina John, amesema licha ya Serikali ya Awamu ya Sita kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, bado kuna mahitaji mbalimbali yanayopaswa kushughulikiwa, ikiwemo uelewa wa jamii kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu.

Ameiomba jamii kuwapa fursa na kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi, akisisitiza kuwa wana uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali kama watu wengine.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Nassir Kirusha, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya huduma kwa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu na afya, kwa kujenga miundombinu inayozingatia mahitaji yao, kama vyoo maalumu na njia za kupita.

Aidha, amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kutowaficha majumbani, bali kuwapeleka shuleni na kuhakikisha wanaandikishwa ili wapate haki ya elimu na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...