Na Nasra Ismail,Geita

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imefanikiwa kusaidia kurejesha jumla ya Shilingi 242,957,748.52 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, chambizo za mifumo, uchunguzi na mashtaka.

Taarifa hiyo imetolewa leo na makamu Mkuu wa TAKUKURU (M) Geita, Alex Mpemba, katika taarifa kwa umma kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.

Katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiasi cha Shilingi 24,658,549.52 zimerejeshwa kutokana na ufuatiliaji wa miradi 38 yenye thamani ya Shilingi 61,526,803,015.26 katika sekta za Elimu, Afya, Barabara, Utawala, Maji na Miradi ya Maendeleo ya Jamii.

Kati ya miradi hiyo, miradi 32 imebainika kuwa na mapungufu madogo ambapo ushauri umetolewa kurekebisha mapungufu hayo, huku miradi 6 ikiwa na kasoro kubwa ambapo hatua za haraka zilichukuliwa.

Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kudhibiti malipo ya Shilingi 2,400,000 yasilipe kwa Mzabuni baada ya kuwasilisha madawati 30 yaliyokuwa yametengenezwa kwa mbao mbichi katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Butambala iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

Pia, kudhibiti malipo ya Shilingi 3,310,000.00 ikiwa ni sehemu ya malipo ya ufundi na vifaa katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mtumishi “2 in 1” katika Zahanati ya Nyarubanga, na kuwasilisha kiasi cha Shilingi 6,874,216.19 kwenye akaunti ya Kamishina wa Kodi za Ndani ambacho kilikuwa hakijawasilishwa katika Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Bukombe.

TAKUKURU Mkoa wa Geita imefanya chambizo 10 za mifumo ikiwemo uchambuzi wa mfumo wa makadirio na makusanyo ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Katika chambizo hizo ziliwekwa maazimio manne ambayo utekelezaji wake katika mwaka 2025/2026 umewezesha kiasi cha Shilingi 14,037,955 kukusanywa.

Katika kutoa elimu kwa umma, TAKUKURU imefanya semina 32 uimarishaji wa Klabu 148, mikutano ya hadhara 38, maonyesho 05 na utoaji wa habari 09.

Hatua hiyo imelenga kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.

Kiasi cha Shilingi 198,161,244.00 kimerejeshwa Serikalini kutokana na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mapato ya ndani (Own Source) zilizokusanywa kupitia mashine za POS na kupitia mfumo wa kielektroniki wa LGRICS.

Fedha hizo ni pamoja na kiasi cha Shilingi 174,782,610.00 kilichodhibitiwa katika akaunti za Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Shilingi 23,378,634.00 kilichorejeshwa katika akaunti za Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Mbogwe, pamoja na kiasi cha Shilingi 6,100,000 kilirejeshwa katika akaunti ya mfuko wa maendeleo ya jamii baada ya fidia ya ardhi kwa eneo ambalo alimilikishwa kabla ya eneo hilo kutwaliwa na mgodi wa Buckreef katika Kijiji cha Mnekezi.

Aidha, jumla ya malalamiko 72 yalipokelewa. Kati ya hayo, malalamiko 57 yalikuwa yahusuyo rushwa, na malalamiko 15 yahusuyo makosa yasiyo ya rushwa. Malalamiko yasiyohusu rushwa yalishughulikiwa kwa kupewa ushauri, huku yale yaliyohusu rushwa yakipelekwa kwa uchunguzi, na mengine yakirudishwa kwenye taasisi za mamlaka husika kwa ufanyiwaji kazi.

Kesi 28 ziliamuliwa ambapo Jamhuri ilishinda kesi zote 28. Katika kipindi hiki kesi 37 mpya ziliunguliwa Mahakamani.

Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, TAKUKURU imejipanga kuongeza kiwango cha kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuimarisha kiwango cha kuelimisha umma katika makundi tofauti ili kuongeza uelewa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi, pamoja na uboreshaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...