-Rais Samia kufungua mkutano mkubwa wa afya ya mama na mtoto Novemba 25, pia kusaini mkataba mpya na wakuu wa mikoa


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

VIFO vitokanavyo na uzazi nchini vimepungua kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 huku pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano navyo vimeshuka kwa asilimia 36, kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

Takwimu hizo zimetolewa leo Novemba 23,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt Ahmad Makuwani, alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Dkt Makuwani amesema mafanikio hayo yametokana na mikataba ya uwajibikaji kati ya Rais na wakuu wa mikoa. Mkataba wa kwanza ulisainiwa mwaka 2018 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "Jiongeze Tuwavushe Salama" na ulihusu afya ya uzazi, mama na mtoto.

Wakati mkataba wa pili ulisainiwa mwaka 2022 na ulihusu lishe ambapo kwa pamoja mikataba hiyo imeongeza uwajibikaji wa viongozi wa mikoa nchini kote.

Akifafanua amesema moja ya mafanikio makubwa ni wodi maalum za watoto wachanga, ambazo zimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025. Kwa mara ya kwanza, wizara imetoa takwimu za watoto waliohudumiwa kwenye wodi hizo.

Amesema watoto 71,000 walilazwa mwaka 2025, na wengine 91,000 kati ya Januari na Septemba 2026. "Tulikuwa hatufanyi vizuri huko nyuma kwa kukosa huduma za watoto wachanga," amekiri Dkt Makuwani.

Ameongeza huduma pia zimesogezwa karibu na wananchi. Kati ya mwaka 2015/16 na 2024/25, zahanati zimeongezeka kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067, na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194. Kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanapata huduma ndani ya kilomita tano kutoka makazi yao.

Kwa upande wa fedha na vifaa, amesema bajeti ya sekta ya afya imepanda hadi shilingi trilioni 3.7 mwaka 2026/27, kutoka Sh.trilioni 2.46 mwaka 2023/24. Pia upatikanaji wa dawa za afya ya uzazi, mama na mtoto umefikia zaidi ya asilimia 85 katika miaka mitatu iliyopita.

“Magari ya kubebea wagonjwa yameongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka 2026. Hospitali zinazosambaza hewa ya oksijeni zimeongezeka kutoka 4 hadi 44.”

Akieleza zaidi amesema mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama, ulioanzishwa mwaka 2020, umesafirisha wagonjwa 250,000 hadi Agosti 2026. Kati yao, asilimia 81 ni akina mama, asilimia 18 ni watoto wachanga, na asilimia moja ni mama na mtoto kwa pamoja.

Ameongeza kwamba huduma za dharura pia zinaratibiwa kupitia makundi ya mawasiliano ya kidijitali (telemedicine) ya halmashauri, mikoa na kanda.

Dkt Makuwani amesema mafanikio hayo hayakutokana na sekta ya afya peke yake. Vijiji vyote 12,318 vimeunganishwa na umeme, ambao ni muhimu wakati wa upasuaji na kuhudumia wagonjwa mahututi.

“Vijiji 10,779, sawa na asilimia 83, vinapata maji safi, hali inayosaidia kuzuia maambukizi. Barabara zinazopitika wakati wote zenye urefu wa kilomita 144,300 zimefupisha safari za rufaa.”

Dk.Makuwani amesema mwitikio wa wajawazito umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2022. Wanaohudhuria kliniki mara ya kwanza sasa ni asilimia 86, kutoka 84. Wanaohudhuria angalau mara nne wamepanda kutoka asilimia 65 hadi 81.

Amesema wanaojifungulia vituoni ni asilimia 85, kutoka 81 huku akieleza chanjo ya tatu ya PENTA imefikia asilimia 96 na ya Surua-Rubella asilimia 94, viwango vilivyo chini kidogo ya zaidi ya asilimia 98 na asilimia 97 za mwaka 2022.

Mafanikio hayo yameipa Tanzania heshima kimataifa. Rais Samia Suluhu Hassan alipewa tuzo ya Goalkeeper ya Gates Foundation Februari 2025, na ni Kinara wa Umoja wa Afrika kwenye huduma za mama na mtoto.

Dkt Makuwani amesema heshima hiyo inawafanya wasaidizi wa Rais "kutembea kifua mbele" kwa kuonyesha umahiri wao barani Afrika.

Mkutano wa tatu wa afya ya uzazi, mama, mtoto na lishe utafanyika Novemba 25 hadi 27, 2026. Umeandaliwa na Wizara ya Afya, OWM-TAMISEMI na wadau wa maendeleo. Rais Samia ndiye mgeni rasmi wa ufunguzi.

Katika mkutano huo, Rais atasaini Mkataba wa Pili wa Uwajibikaji na wakuu wa mikoa.Pia atazindua ripoti ya hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto nchini. “Rais Samia atakabidhi wakuu wa mikoa Mpango wa Nne wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto kama kitendea kazi.”

Ajenda kuu ya mkutano ni kujipanga kufikia malengo ya mwaka 2030. Vifo vya uzazi vinatakiwa kushuka chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinatakiwa kuwa chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000. Vifo vya watoto wachanga vinatakiwa kuwa chini ya 12 kwa kila vizazi hai 1,000.

Dkt Makuwani ametumia mkutano huo kutoa rai kwa vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto, na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili wapate huduma bora bila kuumia kifedha.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...