Na. Vero Ignatus,Michuzi Tv-Arusha

TANZANIA imejizatiti kuendeleza sekta ya utalii, kuimarisha uhifadhi na kuboresha ubora wa huduma, huku ikiweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na ukuaji wa kitaaluma katika sekta hiyo. 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dk Ernest Mjingo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Waongoza Watalii wa Afrika wa mwaka 2026, uliofanyika jijini Arusha.

Dkt Kijaji alisema waongoza watalii ni wadau muhimu katika maendeleo ya sekta hiyo kutokana na maarifa na weledi wao, akiwataka kutumia teknolojia mpya kuboresha huduma na kuimarisha ushindani wa utalii wa Afrika. Alisema sekta hiyo inatoa fursa za ajira, ubunifu na ujasiriamali, hususan kwa vijana na wanawake, ambao wanaweza kushiriki kama waongoza watalii, wakalimani wa tamaduni na mabalozi wa uhifadhi.

Alisisitiza umuhimu wa kuunganisha utalii na uhifadhi endelevu, akitaja vivutio vya Serengeti, Bonde la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na fukwe za Zanzibar kuwa sehemu ya urithi muhimu unaopaswa kulindwa. Aidha, alizitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano, kuoanisha viwango vya taaluma ya uongozaji watalii na kuhakikisha simulizi za historia, tamaduni na mafanikio ya Afrika zinawasilishwa kwa usahihi.

Kwa upande wake, Rais wa Bodi ya Utalii ya Pan Africa, Mariam Lesian, alisema mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake barani Afrika, ukiwakutanisha washiriki wapatao 800 kutoka nchi 38 kwa ajili ya kujadili maendeleo ya utalii, changamoto za kitaaluma na matumizi ya teknolojia zinazoibuka, ikiwemo akili unde (AI).

Bi Mariam Lesian, amesema mkutano wa kwanza unaowakutanisha waongoza watalii kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ni hatua muhimu ya kihistoria katika kuimarisha sekta ya utalii na kutekeleza Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika yenye maono ya Afrika tunayoitaka.

Amesema mkutano huo ni fursa ya kutambua mchango wa waongoza watalii ambao ni mabalozi na walinzi wa vivutio vya utalii, akisisitiza kuwa hakuna sekta ya utalii inayoweza kukamilika bila uwepo wa waongoza watalii wanaowasaidia wageni kufahamu historia, utamaduni na vivutio vya maeneo wanayotembelea.

 "Waongoza watalii ni mabalozi na walinzi wa urithi wa Afrika kwa kuwa wana jukumu la kuwaeleza wageni historia, utamaduni na umuhimu wa vivutio vya bara hilo"Alisema

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania na Chama cha Waongoza Watalii Afrika Mashariki, Dk Robert Max, alisema Tanzania ina zaidi ya waongoza watalii 20,000 waliosajiliwa na kupewa leseni, huku akibainisha changamoto ya baadhi yao kukosa manufaa ya kifedha yanayostahili na uhakika wa mafao ya uzeeni. 

Wadau wengine, akiwemo mwongoza watalii kutoka Kenya, Felix Migoya, na Margaret Samson kutoka Chama cha Waongoza Watalii Kaskazini mwa Tanzania, walisisitiza umuhimu wa kuitangaza Afrika kupitia simulizi zake halisi na kuongeza ushiriki wa wanawake katika taaluma hiyo. 
Dkt Ernest Mjingo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi Utafiti wa Wanyama Pori (TAYARI)

Katibu Mkuu wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania na Chama cha Waongoza Watalii Afrika Mashariki, Dkt. Robert Max,
Rais wa Bodi ya Utalii ya Afrika (Pan-African Tourism Board), Mariam Lesian,



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...