Na Mwandishi Wetu.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeshiriki Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Bandari na Usafirishaji (PMAESA Ports and Maritime Investment Forum & Exhibition 2026), uliofanyika kuanzia Oktoba 28 hadi 30, 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

Ushiriki wa TFS katika mkutano huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa mizigo bandarini, udhibiti wa shehena zinazopita nchini kwenda nchi nyingine (Transit Cargo) na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayohusu biashara ya rasilimali za misitu, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyama na Mimea Pori iliyo Hatarini Kutoweka  (CITES).

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Uhifadhi Mkuu (SCO), Reuben Magandi, aliyewakilisha TFS, alisema wakala huo utatumia fursa na maarifa yaliyopatikana kuboresha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa shehena za mazao ya misitu zinazopitia katika bandari za Tanzania.

Mkutano huo uliandaliwa na Jumuiya ya Usimamizi wa Bandari za Afrika Mashariki na Kusini (PMAESA) na kuwakutanisha wawakilishi wa wizara, taasisi zinazotoa huduma bandarini na mipakani, mawakala wa forodha, wadau wa sekta ya usafirishaji pamoja na nchi wanachama.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uwekezaji katika miundombinu ya bandari, matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, biashara endelevu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Aidha, washiriki walijadili fursa za uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo barabara zinazounganisha nchi wanachama, kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa mizigo, kupunguza ucheleweshaji na kuboresha utoaji wa huduma katika minyororo ya biashara ya kikanda na kimataifa.

Mkutano huo ulihusisha nchi na maeneo wanachama wa PMAESA, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Angola, Botswana, Burundi, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Djibouti, Ethiopia, Eswatini, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe, miongoni mwa nyingine.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...