NA MWANDISHI WETU
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema ushirikiano wake na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark (DIHR) umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha juhudi za kukuza na kulinda haki za binadamu nchini, hususan katika masuala ya biashara na haki za binadamu pamoja na usimamizi wa rasilimali za bahari.
Mwenyekiti wa THBUB, Wakili Dunford George Mpelumbe, amesema hayo alipokutana na ujumbe wa DIHR jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa ushirikiano huo ulioanza mwaka 2017 umewezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo tathmini ya hali ya biashara na haki za binadamu, kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu na kujenga uwezo wa watumishi.
Amesema Tume pia imefanya uchambuzi kuhusu haki za wavuvi wadogo na upatikanaji wa rasilimali za baharini kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa wa jamii za pwani kuhusu haki zao na ushiriki katika maamuzi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuharakisha kupitishwa na kutekelezwa kwa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu, kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko na kuhakikisha haki za binadamu na mazingira zinazingatiwa katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Haki za Binadamu, Biashara na Teknolojia wa DIHR, Bernard Ochieng, ameishukuru THBUB kwa ushirikiano mzuri na kuahidi kuendeleza mahusiano hayo yenye tija.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...