*Yasisitiza wananchi kujiunga na skimu zilizosajiliwa, yataka uwazi wa vifurushi na huduma




Na Said Mwishehe,Michuzi Blog

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewataka Watanzania kujiunga na skimu za bima ya afya zinazotambulika kisheria ili kujikinga na gharama za matibabu, huku ikizionya kampuni na skimu zinazotoa huduma hizo kuhakikisha wananchi wanapewa taarifa sahihi kuhusu vifurushi na stahiki zao.

Mamlaka hiyo imesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu wanapozihitaji bila kukabiliwa na vikwazo vya kifedha, lakini mafanikio yake yanategemea uwazi, uaminifu na usimamizi madhubuti wa watoa huduma.

Akizungumza leo Novemba 16,2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kilichoandaliwa na TIRA chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Kamishna Mkuu wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware, amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, ikiwamo kuhakikisha skimu za umma na binafsi zinatoa huduma kwa kuzingatia sheria na kulinda haki za wanachama.

Amesema wananchi wanapaswa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi za bima zilizosajiliwa na kusimamiwa na TIRA, akisisitiza kuwa bima ya afya ni kinga inayopaswa kununuliwa kabla ya mtu kuugua.

“Bima ya afya ni utaratibu wa kununua kinga kabla ya ugonjwa ili uweze kupata matibabu unapougua. Huwezi kusubiri gari ipate ajali ndipo uanze kutafuta bima,” amesema.

Dk. Saqware amesema wananchi wanaojiunga na NHIF au kampuni binafsi zilizosajiliwa wana haki ya kupata huduma kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa, huku TIRA ikiendelea kusimamia watoa huduma ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao.

Amezitaka kampuni na skimu za bima kuhakikisha kabla ya mwananchi kujiunga, anapewa maelezo yanayoeleweka kuhusu huduma zinazolipiwa, zile ambazo hazijumuishwi, masharti ya matumizi ya bima na utaratibu wa kupata matibabu.

Pia ameonya dhidi ya matumizi ya matangazo na ahadi zinazoweza kuwapotosha wananchi na kuwafanya kujiunga na vifurushi bila kuelewa huduma wanazostahili kupata.

Aidha amezitaja skimu hizo kuweka wazi orodha ya hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazotambuliwa katika utoaji wa huduma ili wananchi waweze kujua wanakoweza kupata matibabu kupitia bima zao.

“Ni muhimu malalamiko ya wanachama kupokelewa, kuchunguzwa na kutatuliwa kwa wakati katika ngazi za kampuni na skimu husika, huku wananchi wanaoshindwa kupata suluhisho wakipewa nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao TIRA kwa hatua zaidi za kiudhibiti.”

Amefafanua jukumu la mamlaka hiyo si kuwa idara ya madai ya kampuni za bima, bali kuhakikisha watoa huduma wanatimiza wajibu wao na kulinda haki za wananchi.

Kuhusu sekta ya bima kukua kwa kasi amesema mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi asilimia 2.11 mwaka 2025, huku mamlaka hiyo ikilenga kufikisha mchango huo asilimia tano ifikapo mwaka 2050.

Amefafanua ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa matumizi ya huduma za bima nchini, ambapo idadi ya watumiaji imeongezeka kutoka milioni 5.6 mwaka 2021 hadi milioni 26.8 mwaka 2025.

“Mafanikio hayo yanaonyesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda mali, afya, biashara na uwekezaji dhidi ya vihatarishi mbalimbali.

“Aidha ajira rasmi katika sekta hiyo zimeongezeka kutoka 3,777 mwaka 2021 hadi 15,568 mwaka 2025, huku matumizi ya huduma za bima kwa kila Mtanzania yakipanda kutoka Sh15,560 hadi Sh67,455 katika kipindi hicho.”

Dkt. Saqware amesema ukubwa wa soko la bima nao umeongezeka, ambapo thamani ya ada za bima zilizokusanywa imepanda kutoka Sh bilioni 911 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.55 mwaka 2025.

Amesema mali za kampuni za bima zimeongezeka kutoka Sh bilioni 979 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.2 mwaka 2025, huku thamani ya mali zilizowekewa kinga ya bima ikipanda kutoka Sh bilioni 367 hadi Sh trilioni 1.29.

Ameongeza sekta hiyo imeendelea kuimarika katika ulipaji wa madai, ambapo takwimu za mamlaka zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya madai hulipwa, huku changamoto zinazobaki zikihusishwa na masuala ya nyaraka na uchunguzi wa udanganyifu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...