-Wananchi milioni 32 wanufaika na mradi wa minara 758 wenye thamani ya Sh.bilioni 126


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kufikisha huduma za simu na intaneti katika kata na vijiji ambavyo havina mawasiliano ya uhakika hasa vijijini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 3,2026 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Albert Richard, alipokuwa akielezea utekelezaji wa miradi mbambali mbele ya wahariri na waandishi wa habari nchini.

Amesema hatua ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga Tanzania ya kidijitali kwa kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, teknolojia ya habari na mifumo inayowawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.

Amesema kwamba mfuko huo umeendelea kutekeleza miradi katika sekta za mawasiliano ya simu, utangazaji, posta na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo bila kujali maeneo wanayoishi.

“Katika miradi ya mawasiliano ya simu, UCSAF imepanga kujenga jumla ya minara 2,324 kupitia awamu mbalimbali, ambapo minara 2,199 imejengwa katika mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kata 2,053 zimefikiwa na huduma hizo.

“Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa ni ujenzi wa minara 758 wenye thamani ya Sh126 bilioni. Mradi huo umelenga kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 713 na vijiji 1,401 vyenye jumla ya wananchi wanaokadiriwa kufikia milioni 32,”amesema Mhandisi Richard.

Ameongeza minara yote 758 imekamilika na kuwashwa, ikiwa ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na kampuni za simu zinazoshiriki katika ujenzi na utoaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo husika.

Pia amesema kupitia mradi huo, minara 169 imekabidhiwa kwa Airtel, 34 kwa Viettel, 261 kwa Yas, 104 kwa TTCL na 190 kwa Vodacom, hatua inayowawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.

Wakati huo huo amesema UCSAF inaendelea kutekeleza mradi wa awamu ya 10 wa ujenzi wa minara 287 katika kata 287 kwa gharama ya Sh29 bilioni. Mradi huo ulizinduliwa Desemba 5, 2025 na unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi 15.

“Hadi sasa minara 65 kati ya 287 imewashwa, sawa na asilimia 23 ya utekelezaji wa mradi huo, huku kazi zikiendelea ili kukamilisha miundombinu iliyobaki na kupanua upatikanaji wa huduma za simu na intaneti katika maeneo yaliyolengwa.

Akizungumzia sekta ya utangazaji, amesema UCSAF imefadhili ujenzi wa vituo 11 vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC), ambavyo vimekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. Ujenzi wa vituo hivyo umegharimu Sh2.5 bilioni.

Ameongeza mfuko huo pia unaendelea na ujenzi wa vituo vingine 26, vitakavyofanya jumla ya vituo vinavyojengwa kufikia 37, vyenye thamani ya Sh.bilioni 15.3, hatua inayolenga kuongeza usikivu wa matangazo ya redio katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu uimarishaji redio za jamii amesema hadi Septemba 2026, UCSAF imewezesha uboreshaji na uanzishwaji wa studio tano pamoja na ujenzi wa minara saba ya redio za jamii kwa gharama ya takribani Sh5.7 bilioni. Aidha, miradi mingine 15 inaendelea kutekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh6.4 bilioni.

Pia amesema mfuko huo pia umeendelea kuunga mkono Shirika la Posta Tanzania kwa kulipatia vifaa vya kisasa vinavyolenga kurahisisha utoaji wa huduma za posta kwa njia ya kidijitali.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...