Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Wathibiti ubora wa shule nchini wametakiwa kutumia maarifa waliyoyapata katika mafunzo ya Shule Salama kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa salama na rafiki kwa wanafunzi, hususan katika masuala ya afya, lishe na ustawi wao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Grace Mbilinyi, wakati wa kufunga mafunzo ya siku nne kwa maafisa hao yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.

Mbilinyi amesema wathibiti ubora wana jukumu muhimu la kubaini changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama na maendeleo ya wanafunzi, kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati na kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu usalama wa watoto shuleni.

Amesisitiza umuhimu wa kufuatwa kwa kalenda za shule na maelekezo rasmi ya Serikali, ikiwemo yale yanayotolewa kutokana na tahadhari za hali ya hewa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo katika Kituo cha Mwanza, Majaliwa Mkalawa, amesema mafunzo hayo yamewafikia maafisa 703 kati ya 722 waliolengwa kutoka mikoa 13, wakiwemo wanaume 438 na wanawake 265.

Amesema mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), kwa lengo la kuongeza uwezo wa maafisa kufanya tathmini za shule na kutoa ushauri wa kuboresha mazingira ya utoaji elimu.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Butimba, Nicholaus Magige, amewataka wathibiti ubora kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kutenganisha mahusiano binafsi na wajibu wa kikazi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi wa ubora wa elimu na kuhakikisha shule zinakuwa mazingira salama kwa ukuaji na maendeleo ya wanafunzi.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...