Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

WAFUGAJI katika Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuboresha ufugaji kwa kuzingatia kanuni za kisasa ili kukidhi vigezo vya masoko ya nje na ndani ya nchi, ikiwemo kupanda majani ya malisho, kutoa chanjo kwa mifugo na kutumia mfumo wa ufugaji wa ndani (zero grazing).

Hatua hiyo inalenga kuongeza ubora na uzalishaji wa mifugo, kudhibiti magonjwa pamoja na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Moses Magogwa, Novemba 16, 2026, wakati akizindua awamu ya pili ya zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kwa ruzuku, eneo la Mtakuja, Kata ya Pangani, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhil Nkurlu.

Magogwa alisema wafugaji wamekuwa wakikosa fursa za soko la nje kutokana na kutofikia vigezo vinavyohitajika, huku akitaja uwepo wa viwanda vya kuchakata nyama vya Tan Choice na Union Meat kuwa fursa inayopaswa kutumiwa na wafugaji wa eneo hilo.

Alisema viwanda hivyo vimekuwa vikikabiliana kutopata mifugo inayokidhi mahitaji yake, hivyo ni muhimu wafugaji kuboresha mbinu za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mifugo inayozalishwa.

Alieleza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuja na mpango wa chanjo na utambuzi wa mifugo kwa ruzuku ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali, ikiwemo homa ya mapafu kwa ng'ombe, pamoja na kuweka alama za utambulisho zitakazosaidia kudhibiti wizi wa mifugo.

Aidha, Magogwa aliwataka wataalamu wa mifugo kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa, ikiwemo kuwatembelea katika shamba la mbegu za majani lililopo Vikuge, Kata ya Soga, ili kujifunza namna ya kupanda na kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo yao na hivyo kupunguza tabia ya kuhama hama kutafuta chakula.

Kwa upande wake, mfugaji wa Mtaa wa Mtakuja, Twalibu Selemani, alisema mpango huo wa miaka mitano ni mkombozi kwao kwa kuwa utasaidia kukabiliana na changamoto ya vifo vya mifugo vinavyotokana na magonjwa pamoja na wizi unaochangiwa na kutokuwepo kwa alama za utambulisho.

Naye Daktari wa Mifugo wa Manispaa ya Kibaha, Chiza Martin, alisema Serikali imetoa chanjo kwa ruzuku pamoja na kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Alisema kabla ya kuanza kwa mpango huo, wafugaji walikuwa wakichangia Sh 1,500 kwa chanjo ya ng'ombe, Sh 300 kwa mbuzi na kondoo, huku chanjo ya kuku ikitolewa bure.

Alifafanua kuwa chanjo hizo zinalenga kukabiliana na magonjwa ya homa ya mapafu, sotoka na mdondo (kideli).

Alisema Manispaa ya Kibaha ina jumla ya ng'ombe 85,000, mbuzi 65,000 na kuku 300,000, huku katika awamu hii Serikali ikiwa imeanza kutoa chanjo kwa ng'ombe 2,000, kuku 150,000 na mbuzi 1,500.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...